Kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu nchini Ethiopia, watu wengi waliuawa na kujeruhiwa katika siku za hivi karibuni huko Amhara, kaskazini mwa nchi hiyo. Tangu mwaka 2023, mapigano kati ya jeshi la serikali na Fano – wanamgambo wa kikanda – yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika eneo hili, la pili kwa idadi kubwa ya watu nchini Ethiopia.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwanahabari wetu mjini Addis Ababa, Marlène Panara

Tangu mwishoni mwa mwezi Septemba, mzozo unaoendelea katika jimbo la Amhara umeongezeka: hasa katika eneo la Wollo Kaskazini, takriban kilomita 550 kutoka Addis Ababa, mashambulizi yamesababisha hasara nyingi. Wiki hii, Shirika la Msalaba Mwekundu lilipeleka dawa na vifaa vya matibabu katika vituo vya afya karibu na miji ya Lalibela na Woldiya, wakiwatibu watu 250 waliojeruhiwa vibaya.

Mapigano makali pia yameshuhudiwa kusini kidogo huko Gashena. Kwa saa chache, Fano walichukua udhibiti wa mji kwa muda mfupi kabla ya kurudi nyuma. Mnamo Septemba 27, shambulio la ndege zisizo na rubani, wakati huu lililofanywa na jeshi, kwenye kituo cha afya cha Sanqa, Kaskazini mwa Wollo, liligharimu maisha ya watu wanne, akiwemo mwanamke mjamzito. Mlipuko pia ulijeruhi makumi ya wengine, wengi wao wakiwa wagonjwa na wafanyikazi wa afya.

Kwa raia, matokeo ya mzozo huu, ulioanza mwezi Aprili 2023, ni mbaya sana. Upatikanaji wa huduma za afya ni mdogo, na kutokana na vituo vingi vya ukaguzi, vinavyodhibitiwa na Fano au jeshi, kutembea katika jimbo la Amhara ni vigumu sana. Hakuna idadi rasmi ya vifo, lakini kulingana na data kutoka kwa shirika la ACLED lililonukuliwa na serikali ya Uingereza, zaidi ya watu 9,000 walifariki kati ya mwezi Aprili 2023 na mwezi Juni 2025, raia na wapiganaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *