
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imefuta maombi ya mjane, Evelyne Chilumba ya kuomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Evelyne kupitia wakili wake, Ferdinand Makore alikuwa amefungua maombi namba 111645 ya mwaka 2026 akitaka apewe kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga agizo analodai lilitolewa na Chalamila, kuhusu nyumba anayoishi.
Katika shauri hilo, Evelyne alimshitaki Chalamila kwa jina lake na kwa wadhifa wake, akimuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa pili. Pia aliwaunganisha Godfrey Shuma na Callista Shuma kama wadaawa muhimu.
Kwa mujibu wa maombi yake, Evelyne aliwasilisha kiunganishi cha video ya YouTube akidai Chalamila alitoa maelekezo ya kuondolewa kwake katika nyumba iliyopo katika Kiwanja Na. 317, Regent Estate jijini Dar es Salaam, ambayo alisema ameishi tangu kifo cha mumewe, Raphael Chiomba, mwaka 1993.
Hata hivyo, katika uamuzi uliotolewa Juni 23, 2026 na kuchapishwa katika tovuti ya TanzLII Juni 24, 2026, Jaji Arnold Kirekiano amekubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa Chalamila.
Jaji Kirekiano amesema maombi hayo hayakuungwa mkono na nyaraka za kutosha zinazowezesha mahakama kutathmini nafuu iliyokuwa ikiombwa.
“Ninaona hoja ya kwanza ya pingamizi kuwa ni halali kwa kiwango ambacho ombi halijaungwa mkono na nyenzo za kutosha ili kuamua unafuu unaotafutwa kwa kuzingatia sifa zake. Maombi haya hayafai na yamefutwa bila gharama,” amesema Jaji Kirekiano.
Akifafanua zaidi, Jaji amesema mwombaji aliwasilisha kiunganishi cha YouTube akikusudia kukitumia kama ushahidi wa taarifa rasmi ya umma iliyotolewa na mjibu maombi wa kwanza.
“Ni jambo moja kuwa na matangazo ya uamuzi au maagizo kutoka kwa ofisi ya umma kuwasilishwa kwa umma, na jambo jingine kuwa na nakala ya maandishi ya uamuzi huo kutoka kwa ofisa husika. Hilo la pili ndilo linalofaa kwa madhumuni ya mapitio ya mahakama,” amesema.
Ameongeza kuwa ilitarajiwa mwombaji angechukua hatua za kupata nakala ya uamuzi huo kutoka kwa ofisi ya mlalamikiwa kabla ya kuwasilisha maombi mahakamani.
“Ofisi ya umma inayofanya uamuzi inatarajiwa kuwa na kumbukumbu sahihi ili wahusika walioathirika waweze kuzipata na, ikihitajika, zitumike katika mchakato wa mapitio ya mahakama,” amesisitiza.
Kutokana na uchambuzi huo, Jaji amesema pingamizi la kwanza lilikuwa na msingi kwa kuwa maombi hayo hayakuambatanishwa na nyaraka za kutosha kuthibitisha uwepo wa uamuzi unaolalamikiwa na hivyo kuyafuta bila gharama, huku kila upande ukibeba gharama zake.
Pia, amefuta amri ya muda iliyokuwa imetolewa Mei 15, 2026 iliyokuwa ikizuia utekelezaji wa agizo linalodaiwa kutolewa na RC Chalamila.
Pingamizi lilivyowasilishwa
Katika hati yake ya kiapo, Evelyne ameeleza kuwa yeye ndiye msimamizi wa mali za marehemu mumewe na kwamba, ameendelea kuishi katika nyumba hiyo tangu mwaka 1993.
Kwa upande wao, Godfrey Shuma na Callista Shuma wamedai kuwa wao ndio wamiliki halali wa kiwanja hicho kwa mujibu wa hati ya umiliki Na. CT 21221 tangu mwaka 1995.
Evelyne alidai kuwa Mei 15, 2026 RC Chalamila alitoa maelekezo ya kuondolewa kwake kwa nguvu katika nyumba hiyo aliyodai kuishi kwa zaidi ya miaka 30, hivyo akaomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga maamuzi, maelekezo na matendo ya mkuu huyo wa mkoa.
Hata hivyo, maombi hayo yalipingwa kupitia pingamizi la awali lenye hoja sita. Hoja ya kwanza, ambayo ndiyo ilikubaliwa na mahakama, ilidai kuwa maombi hayo yalikiuka masharti ya msingi ya mapitio ya mahakama kwa kutowasilisha uamuzi unaotakiwa kufanyiwa mapitio.
Pingamizi hilo liliwasilishwa na Chalamila pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ayoub Sanga na kusikilizwa kwa njia ya maandishi.
Akijenga hoja zake, Sanga amesema kiunganishi cha YouTube kilichowasilishwa na mwombaji hakiwezi kuchukuliwa kuwa uamuzi rasmi unaoweza kufanyiwa mapitio ya mahakama.
Amesema mahakama haiwezi kutoa amri ya kufuta uamuzi ambao haujathibitishwa kuwepo wala kuwasilishwa rasmi mbele yake.
Kwa upande wake, wakili Dickson Mtogosewa aliyewawakilisha wadaawa muhimu, ametilia shaka mamlaka ya mahakama kusikiliza maombi dhidi ya wateja wake akisema si vyombo vya umma wala hawana mamlaka ya umma yanayoweza kuwa msingi wa shauri la mapitio ya mahakama.
Akijibu hoja hizo, wakili Makore amerejea uamuzi mbalimbali wa mahakama na vifungu vya sheria akisisitiza kuwa hakuna takwa la kisheria linalomlazimu mwombaji kuambatanisha uamuzi unaolalamikiwa katika hatua ya kuomba kibali.
Amedai pia kuwa suala la kuwepo au kutokuwepo kwa uamuzi huo lilipaswa kujadiliwa katika shauri kuu na si katika hatua ya maombi ya kibali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Kirekiano alikubaliana na pingamizi la kwanza na kuhitimisha kuwa maombi hayo hayakuwa na nyaraka za kutosha kuwezesha mahakama kutathmini nafuu iliyokuwa ikiombwa.