
Marekani imekaribisha siku ya Ijumaa wito wa mamlaka ya Kongo kwa wapiganaji wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) kuweka chini silaha zao, ikiona kuwa ni hatua madhubuti katika utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa Washington kati ya DRC na Rwanda.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Tunakaribisha wito wa DRC kwa makundi yote ya FDLR kuweka chini silaha zao na kujisalimisha, kwa mujibu wa Mkataba wa Amani wa Washington, ulioimarishwa na agizo la operesheni la Oktoba 1,” alisema Massad Boulos, mshauri mkuu wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. “Hatua hii madhubuti inaendeleza utekelezwaji wa Makubaliano ya Amani ya Washington, kuwezesha wakimbizi kurejeshwa nyumbani, kurejesha mamlaka ya serikali, na kuimarisha utulivu katika eneo la Maziwa Makuu,” aliongeza.
Wito wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC), uliyotolewa siku ya Ijumaa, unayataka makundi yote ya FDLR kujisalimisha kwa mamlaka ya Kongo au MONUSCO kwa nia ya kuwarejesha Rwanda. FARDC pia ilionya dhidi ya upinzani wowote, ikisisitiza kwamba “kupokonya silaha kwa kulazimishwa au kutumia nguvu” kunaweza kutekelezwa kwa mujibu wa masharti ya Mkataba wa Washington.
Mamlaka ya kijeshi ya Kongo pia imepiga marufuku wanajeshi wao kushirikiana na FDLR, chini ya adhabu ya vikwazo vikali, na wametoa wito kwa watu kujitenga na waasi hao wa Rwanda.
Utaratibu wa sasa wa utendaji kazi (OPORD) unatokana na maamuzi yaliyochukuliwa katika mkutano wa tatu wa Kamati ya Pamoja ya Ufuatiliaji ya Mkataba wa Washington, ambayo inatoa mtazamo wa hatua kwa hatua wa kuangamiza FDLR na kuondoa hatua za ulinzi za Rwanda.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje, kikao kijacho cha kamati ya pamoja ya makubaliano hayo kimepangwa kufanyika Oktoba 21 na 22, kufuatia mkutano wa Mfumo wa Pamoja wa Kuratibu Usalama (JSCM).
Mkataba wa Amani wa Washington ambao ulitiwa saini chini ya mwamvuli wa Washington, unakamilisha mchakato wa Doha, mipango miwili ya kidiplomasia inayolenga kuleta utulivu mashariki mwa DRC baada ya miji ya Goma na Bukavu kuanguka mikonononi mwa waasi wa M23 na kushindwa kwa Mchakato wa Luanda.