Uholanzi. Mshambuliaji wa Uholanzi, Cody Gakpo (26) alifanya vizuri katika Kombe la Dunia 2022 Qatar, jambo lililoishawishi Liverpool kumsajili kwa dau la Pauni 37 milioni akitokea PSV ya nchini kwao Uholanzi.

Hata hivyo, Gakpo hakutua katika viunga vya Anfield akiwa peke yake, bali aliongozana na mpenzi wake wa kitambo, Noa van der Bij, 26, ambaye amekuwa shabiki yake kwa muda mrefu  tangu Uholanzi hadi sasa Ligi Kuu England.

Ndani ya muda mfupi, Gakpo ametengeneza jina kubwa katika ulimwengu wa soka lakini mbali na kazi yake, kuna upande mwingine wa maisha yake unaovutia, nao ni uhusiano wake na Noa.

Mrembo huyo amekuwa msaada mkubwa kwa Gakpo kwa sababu ya kuwa karibu na maisha yake ya soka ila siku zote wanapendelea kuweka uhusiano wao kuwa wa faragha ili kuepuka athari hasi za umaarufu.

Kinachojulikana na wengi kuhusu Noa, ni kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Gakpo kwani katika mechi nyingi za Liverpool au timu ya Taifa ya Uholanzi, ameonekana mara kwa mara akimshangilia mpenzi wake huyo.

Mathalani wakati wa michuano ya Kombe la Dunia 2022 ambako Gakpo alifunga mabao matatu katika michezo mitano, Noa alikuwepo uwanjani akimuunga mkono kwa moyo wote.

Ingawa hakuna taarifa nyingi kuhusu mwanzo wa uhusiano wao kwa undani, lakini vyombo vya habari vya Uholanzi vinaripoti walianza kuwa pamoja tangu Desemba 2020.

Walikutana wakiwa Uholanzi kwa kuwa wote wanatokea eneo moja na hata uhusiano wao ulianzia nchini humo. Na kwa mara ya kwanza wawili hao kuonekana hadharani kama wapenzi ilikuwa katika mchezo wa soka.

Tangu wakati huo Cody na Noa wamejenga uhusiano unaoongozwa na upendo, uelewano na usaidizi wa dhati baina yao. Wanaendelea kukua pamoja, wakiwa na matumaini ya kudumisha ukaribu wao kwa muda mrefu zaidi.

Ikiwa ni takribani miaka mitano ya uhusiano wao, mnamo Aprili 25, Noa alijifungua mtoto wake wa kwanza na Cody Gakpo, ambaye waliamua kumpa jina la Samuel Seth.

Wapenzi hao wamekuwa wakishirikiana sana kwenye mitandao ya kijamii, wakiposti picha za familia yao, sherehe na hata nyakati zao maalum. Ingawa wanaposti picha zao, wanajua jinsi ya kudumisha faragha katika uhusiano wao.

Mnamo Mei, wawili hao walienda mapumzikoni Falme za Kiarabu (UAE), katika picha alizoposti, Noa alionekana akifurahia hali ya hewa huku Samuel akitembelea gari la watoto.

Noa anatokea Gorinchem nchini Uholanzi na amekulia huko kwa muda mrefu wa maisha yake. Amezaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo, ingawa taarifa kuhusu wazazi wake au ndugu zake hazijulikani.

Noa alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Avans University of Applied Sciences, kilichopo katika jiji la Breda ambako alipata shahada ya usimamizi wa fedha.

Baada tu ya kumaliza masomo, alijiunga na sekta ya mitindo, na kwa sasa akifanya kazi kama mratibu katika kampuni ya Cachet Models ambayo inajihusisha na masuala ya mitindo na urembo.

Mbali na kazi hiyo pamoja na taaluma yake, Noa pia ni mwanamitindo wa mtandaoni mwenye mafanikio akiwa na wafuasi zaidi ya 44,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, kutokana na shughuli zake za kibiashara na matangazo anayofanya mitandaoni, utajiri wake unakadiriwa kufikia zaidi ya Dola 1 milioni, wastani wa Sh407 milioni.

Noa anaonekana anapenda maisha ya kifahari kwani amekuwa akiposti picha akiwa katika maeneo mbalimbali ya kifahari duniani kama Monaco, Ibiza, Saint Tropez na Curacao.

Mnamo Januari, Gakpo alisafiri na kikosi cha Liverpool kwenda mji alikozaliwa, Eindhoven, kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL) dhidi ya PSV.

Kutokana na safari ya Gakpo, Noa hakutaka kubaki nyumbani peke yake, aliamua kujivinjari nje ya Uingereza pamoja na marafiki zake wakisafiri hadi Cape Town, Afrika Kusini.

Wakiwa huko kwa Madiba, walitembelea eneo la Camps Bay ambalo ni maarufu kwa fukwe zake, migahawa ya vyakula vya baharini na mandhari maridadi ya milima ya Twelve Apostles.

Kupitia Instagram, Noa aliposti picha wakifurahia maisha ya huko hadi kumgusa mwanamitindo Saffie Khan, mpenzi wa kiungo wa Liverpool, Curtis Jones, aliyeacha emoji ya tabasamu katika posti hiyo.

Familia hizo zimekuwa na ukaribu, Jones aliwahi kufichua kuwa yeye na mpenzi wake Saffie walikuwa na urafiki zaidi na Gakpo na Noa hasa kipindi wakijiandaa kuwa wazazi kwa mara ya kwanza.

“Mimi huwa mmoja wa wachezaji wanaowahi kufika uwanjani kwa ajili ya mazoezi. Kisha Gakpo na wengine wanawasili, basi tunaanza mazungumzo ya hapa na pale,” alisema Jones na kuongeza;

“Mimi na Gakpo tuko karibu sana, tunatumia muda pamoja. Wapenzi wetu pia wanaongea mara kwa mara. Kwa kuwa yeye tayari ana mtoto, anamsaidia mpenzi wangu kwa mambo kadhaa. Yeye ni kama kaka yangu,” alieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *