Senegal na Ivory Coast zimekamilisha idadi ya timu tisa zitakazowakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia mwakani baada ya kuibuka na ushindi mnono katika mechi za mwisho za makundi yao jana Jumanne, Oktoba 14, 2025.

Ushindi katika mechi hizo umezifanya Senegal na Ivory Coast kuongoza makundi yao na hivyo kuungana na timu nyingine saba ambazo tayari zimeshafuzu Kombe la Dunia.

Katika Uwanja wa Me Abdoulaye Wade jijini Diamniadio, wenyeji Senegal walijihakikisha uongozi wa kundi B kwa kuitandika Mauritania mabao 4-0.

Ushindi huo umeifanya Senegal kufikisha pointi 24, mbili zaidi ya zile za DR Congo iliyomaliza katika nafasi ya pili na hivyo kuwa na uhakika wa kuwepo Canada, Mexico na Marekani kwenye Kombe la Dunia mwakani.

Walioizamisha Mauritania ni Sadio Mane ambaye amepachika mabao mawili na Iliman Ndiaye na Habib Diallo ambao kila mmoja amefunga bao moja.

Hii ni mara ya nne kwa Senegal kufuzu Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo mwaka 2002, 2018 na 2022.

Jijini Abidjan katika Uwanja wa Olimpiki wa Alassane Ouattara, wenyeji Ivory Coast wamejihakikishia uongozi wa kundi F na tiketi ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kenya.

Franck Kessie, Yan Diomande na Amad Diallo yametosha kuifanya Ivory Coast kumaliza ikiwa kinara wa kundi ikiwa na pointi 26 huku Gabon ikimaliza ya pili na pointi zake 25.

Matokeo ya mechi za jana Kufuzu Kombe la Dunia

Shelisheli 0-7 Gambia

Algeria 2-1 Uganda

Guinea 2-2 Botswana

Nigeria 4-0 Benin

Afrika Kusini 3-0 Rwanda

Somalia 0-1 Msumbiji

Gabon 2-0 Burundi

Ivory Coast 3-0 Kenya

Morocco 1-0 Congo

Senegal 4-0 Mauritania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *