
Kauli ya Katibu Mkuu imetolewana msemaji wake Stéphane Dujarric wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo Alhamisi Oktoba 16 jijini New York, Marekani.
“Guterres ametambua uamuzi wa Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika, (AU) wa kusitisha ushiriki wa taifa hilo kwenye shughuli zote za Muungano huo, Vyombo vyake pamoja na taasisi zinazohusiana hadi pale utawala wa kikatiba utakaporejeshwa nchini humo,” amenukuliwa Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu amesihi wadau wote wa Madagascar, wakiwemo vijana, kushirikiana ili kupatia suluhisho changamoto zote zinazosababisha ukosefu wa utulivu nchini humo.
Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi za kitaifa katika kufanikisha kufikia lengo hilo kwa kushirikiana na AU, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na wadau wengine wa kimataifa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari tarehe 12 Oktoba kikosi mahsusi cha kijeshi kiliungana na waandamanaji na kuasi na kisha Rais Andry Rajoelina akakimbia nchi siku iliyofuatia kwa madai ya kwamba kulikuwa na mpango wa kumuua.
Tarehe 14 Oktoba Rais huyo akiwa na mpango wa kuvunja Bunge kutoka mafichoni, Bunge hilo hilo lilipiga kura na kumfungulia mashtaka kwa kutelekeza wajibu wake.
Hatua hiyo ilifuatiwa na kikosi maalumu cha jeshi, CAPSAT kutangaza kutwaa udhibiti wa serikali, kusitisha takribani taasisi zote za kisiasa na kisha Kanali Michael Randrianirina kuteuliwa kuwa kiongozi wa muda.