Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Chakula Duniani ni “Kwa Pamoja kwa Chakula Bora na Mustakabali Bora,” imeangazia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wote.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake wa siku hii alioutoa kwa njia ya video amesema, “Miaka themanini iliyopita, katika dunia iliyosambaratishwa kwa vita, nchi zilikutana kukabiliana na njaa. Miongo kadhaa tangu wakati huo, dunia imepiga hatua kubwa. Lakini bado majanga yanyoonesha kuwa hatuwezi kubweteka iwapo tunataka kuendeleza mafanikio tuliyopata. Tuna mbinu, ufahamu, rasilimali za kutokomeza njaa, na kupatia kila mtu chakula kizuri na chenye afya. Tunachohitaji ni umoja.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu akitoa hotuba yake wakati wa Ufunguzi Mkuu wa WFF kwenye makao makuu ya FAO mjini Rome.
Njaa haina mipaka: Mkuu wa FAO
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, ambaye ndiye mwenyeji wa sherehe hiyo, amezitaka nchi kuungana kukabiliana na changamoto za chakula duniani.
“Uwepo wenu hapa leo ni ishara halisi kwamba njaa haina mipaka,” amesema. “Viongozi wa dunia na watu kila mahali lazima waungane kwa imani ya pamoja kwamba haki ya kupata chakula ni haki ya msingi ya binadamu, na kwamba amani ni sharti la msingi la uhakika wa chakula.”
Hafla hiyo imehudhuriwa na wakuu wa nchi na wawakilishi kutoka kote ulimwenguni, akiwemo Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Han Jun kutoka China, aliyesoma ujumbe wa pongezi kutoka kwa Rais Xi Jinping akilisifu Shirika la FAO kwa “mafanikio makubwa katika kipindi cha miongo minane.”
Papa Leo XIV akitoa hotuba yake wakati wa sherehe za Siku ya Chakula Duniani duniani na maadhimisho ya miaka 80 ya FAO.
Papa Leo XIV atoa wito wa uamsho wa kimaadili
Katika hotuba yake kuu, Papa Mtakatifu Leo XIV alitoa mwito wa dhati wa kuamsha dhamira ya pamoja ya kumaliza njaa na kuimarisha amani duniani.
“Miaka themanini baada ya kuanzishwa kwa FAO, dhamiri zetu zinapaswa tena kutuuliza kuhusu janga la kudumu la njaa na utapiamlo,” amesema akiongeza kuwa “Katika kipindi cha kihistoria kilichojaa migawanyiko na migogoro, kuwa wamoja kwa dhamira ya ushirikiano si tu wazo zuri, bali ni wito thabiti wa kuchukua hatua.”
Maneno ya Papa yamegusa wengi katika mwaka ambao umeshuhudia ongezeko la uhaba wa chakula duniani kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na misukosuko ya kiuchumi.
Wakulima wadogo nchini Sierra Leone wakionesha mboga walizolima.
Viongozi wa dunia wathibitisha msaada wao
Miongoni mwa waliohudhuria maadhimisho hayo walikuwa ni Mfalme Letsie wa III wa Lesotho, Malkia Letizia wa Hispania, Rais wa Uruguay Yamandú Orsi Martínez, na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kupitia ujumbe wa video, amelaani “utumiaji wa njaa kama silaha” na kutoa wito wa kuongeza uwekezaji katika mifumo endelevu ya chakula.
Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Italia na Waziri wa Mambo ya Nje, Antonio Tajani, amesema kuwa Italia inajivunia kuwa mwenyeji wa FAO, “taasisi muhimu ya ushirikiano wa kimataifa na alama ya matumaini kwa mamilioni ya watu duniani.”
FAO yaanisha urithi wake kwa ubunifu mpya
Kama sehemu ya maadhimisho hayo, FAO imezindua Jumba la Makumbusho na Mtandao wa Chakula na Kilimo (FAO MuNe) kwa ushirikiano na Rais wa Italia, Sergio Mattarella, likiwa wazi kwa umma na lenye eneo la zaidi ya mita za mraba 1,300.
Jumba hilo linaonyesha historia na mustakabali wa mifumo ya chakula duniani kupitia maonyesho ya kielimu na ya mwingiliano.
Pia, huduma ya posta ya Italia imezindua stempu maalum kuadhimisha miaka 80 ya FAO, ikitambua ushirikiano wa muda mrefu kati ya Italia na shirika hilo. Maonesho ya wazi ya kwanza ya FAO, Kutoka Mbegu Hadi Chakula, yamevutia zaidi ya wageni 7,000 yakionesha ubunifu, mila na tamaduni zinazohusiana na uzalishaji wa chakula duniani.
Wauzaji wanauza mazao katika soko la Cotacachi, Ecuador.
Jukwaa la chakula duniani: Njia na hatua madhubuti
Siku ya Chakula Duniani 2025 imehitimishwa na Jukwaa la Chakula Duniani (World Food Forum – WFF), tukio la kila mwaka la FAO linalowaleta pamoja vijana, wanasayansi, wawekezaji, wakulima na viongozi wa jamii za asili.
Kupitia nguzo zake kuu ambazo ni Hatua za vijana duniani, Jukwaa la Sayansi na Ubunifu, na Jukwaa la Uwekezaji la mkono-kwa-Mkono washiriki wamejadili njia za kujenga mifumo ya chakula yenye tija, usawa na mnepo.
FAO ikiingia katika muongo wake wa tisa, Mkurugenzi Mkuu Qu amesisitiza dhamira ya shirika hilo akisema “Lazima tuchukue hatua kwa pamoja kwa mikono iliyo shikamana kuhakikisha dunia isiyo na njaa, ambapo kila mtu anaweza kupata chakula chenye afya na kwa bei nafuu, leo na kwa vizazi vijavyo.”