London, England. Kocha mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amempongeza Leandro Trossard kwa kitendo cha kuisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi muhimu dhidi ya Fulham, kwenye mechi ya jana Jumamosi, Oktoba 19, 2025.
Trossard alifunga bao la ushindi kwenye mechi hiyo dakika ya 58, na kuiwezesha klabu hiyo ya Kaskazini mwa London kuendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya EPL kwa kufikisha pointi 19.
Arteta amesema juhudi na kujituma kwa kikosi chake vimekuwa chachu ya kufanikisha mpango wa matokeo mazuri kwenye mechi ya jana huku akimtaja Trossard kama ‘mchawi’ na ‘silaha kubwa’ kwa Arsenal.
“Trossard ana kipaji cha kipekee cha kuleta maajabu katika wakati ambao timu inayahitaji zaidi, na ile hali ya kujua tu mahali pa kuwa na wakati wa kuwa pale, ni sifa kubwa sana kwa timu yetu, ni silaha kubwa kwetu.
“Alicheza vizuri sana katika wiki za hivi karibuni, na sasa tuna wachezaji wengi walio katika hali nzuri kiakili na kimchezo, jambo ambalo ni zuri sana kuliona.”
Ushindi huo dhidi ya Fulham umekuwa wa kwanza katika kipindi cha mechi saba ndani ya siku 21 kwa vijana wa Arsenal, huku wakitarajia kumenyana na Atletico Madrid kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa keshokutwa Jumanne, kwenye Uwanja wa Emirates.
Arsenal itakuwa na matumaini ya kuendeleza mwanzo mzuri kwenye kampeni yao ya Ulaya, baada ya kushinda mechi mbili mfululizo kwa mabao 2-0, dhidi ya Athletic Bilbao na Olympiacos.
Hata hivyo, mlolongo huu wa mechi unatarajiwa kujaribu kwa kina, kikosi kipya cha Arsenal, huku wachezaji muhimu kama nahodha Martin Ødegaard, Noni Madueke, na Kai Havertz wakiwa nje kwa majeraha.
“Tunajua ratiba ilivyo na mzigo wa mechi hauwezi kubadilika, na mazingira ya sasa yanahitaji kuwa na kikosi kipana. Timu zote kubwa ziko katika hali kama hii, na tutalazimika kuisimamia vyema, kuwajali wachezaji, na hasa kuhakikisha tunapata kiwango bora zaidi kutoka kwao.” amesema Arteta.