Kwa mujibu wa WMO idadi ya nchi zenye mifumo ya tahadhari za mapema kwa ajili ya majanga ya tabianchi imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita lakini bado mamilioni ya watu hawana ulinzi dhidi yah atua hiyo muhimu.

Ndiyo maana shirika hilo limewakutanisha mawaziri na wataalamu kutoka nchi wanachama 193 kuharakisha mpango wa Tahadhari za Mapema kwa Wote, uliozinduliwa mwaka 2022 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres unatekelezwa kwa vitendo.

Katika mkutano huo Celeste Saulo Katibu Mkuu wa WMO amesema “Miaka 75 iliyopita, Shirika la WMO lilianzishwa kutokana na ukweli kwamba hali ya hewa, maji na tabianchi havina mipaka ya kitaifa. Ushirikiano wa kimataifa katika uchunguzi na utabiri ni wa lazima, kwa sababu hakuna nchi inayoweza kufanya hivyo peke yake.”

Athari za mabadiliko ya tabianchi Sindh, Punjab

© UNICEF Pakistan

Athari za mabadiliko ya tabianchi Sindh, Punjab

Ripoti mpya ya WMO, iliyopewa jina Tahadhari za Mapema kwa Wote Mtazamo wa Dunia, inaonesha kuwa licha ya maendeleo makubwa katika ubadilishanaji wa takwimu na utabiri wa kidijitali, bado kuna mapengo makubwa, hasa katika nchi maskini na visiwa vidogo vinavyoendelea.

Celeste amesisitiza kuwa “Tahadhari za Mapema kwa Wote sasa siyo mpango tena, bali ni nembo ya mshikamano wa dunia. Pamoja, tunaokoa maisha, tunaunda sera, na kuimarisha mnepo.”

Takwimu za shirika hilo zinaonesha uzito wa changamoto. Katika miaka 50 iliyopita, WMO inasema majanga yanayohusiana na hali ya hewa na maji yamesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni mbili huku asilimia 90 kati yao ni katika nchi zinazoendelea.

Na ingawa mataifa 108 sasa yana mifumo ya tahadhari za majanga mchanganyiko, shirika hilo linasema viwango vya vifo bado ni mara sita zaidi katika maeneo yasiyo na mifumo hiyo.

Kaunti ya Turkana, kaskazini mwa Kenya, hukumbwa na ukame mara kwa mara.

© UNCCD/Mwangi Kirubi

Kaunti ya Turkana, kaskazini mwa Kenya, hukumbwa na ukame mara kwa mara.

WMO inasema teknolojia mpya ikiwemo akili mnemba na matumizi ya takwimu za setilaiti kwa wakati halisi zinabadilisha uwezo wa utabiri, lakini pengo la kidijitali bado linawaacha wengi wakiwa hatarini.

“Mafanikio ya Tahadhari za Mapema kwa Wote hayapimwi kwa ripoti au maazimio, anasema Celesto bali kwa maisha yanayookolewa na riziki zinazolindwa. Tunapoelekea mwaka 2027, hebu tuongeze juhudi kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa bila ulinzi.”

Mkutano huo Maalum wa WMO utaendelea wiki nzima mjini Geneva, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitarajiwa kuhutubia siku ya Jumatano.
Shirika la WMO wakati likiadhimisha miaka 75 ya kile linachoita Sayansi kwa Vitendo  linataka kuhakikisha sayansi hiyo inawafikia wote, kabla ya majanga kutokea.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *