Peter Nyanda, ambaye ni afisa kutoka UNDP nchini Tanzania amesema hayo akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akitaja moja a mafanikio kuwa ni mipango ya utekelezaji wa dhana hiyo kila mkoa kwa kutambua hatua za haraka, fursa, na jinsi ya kupata uwekezaji.

Kiwanda cha Dangote kinatumia taka kama chanzo cha nishati

Halikadhalika UNDP imefanikiwa kuwatambua wadau katika uchumi rejeshi na wabunifu katika maeneo ya viwanda akitoa mfano wa kiwanda cha Dangote Mtwara.

Amesema kiwanda hicho kinatumia taka kwa ajili ya kuwasha mitambo yake kwa matumizi mbalimbali.

Pamoja na hayo matarajio ni kufanya majadiliano na wafadhili na wadau wa maendeleo, hasa sekta binafsi, ili kupata rasilimali kwa ajili ya uwekezaji.

“Vile vile kuanzisha vituo vya ubunifu na ubora katika maeneo ya miundombinu. Na vituo vya kutenganisha taka. Kuna juhudi za kukuza mtindo wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na taasisi za kifedha ambao utahakikisha mitaji au rasilimali zinapatikana kusaidia kukuza biashara hizo,” amesema Nyanda.

UNDP kubisha hodi mikoa mingine pia

Nyanda ameongeza kuwa juhudi hizi hazitaishia tu katika mikoa miwili iliyotajwa, ambayo ni Tanga na Mtwara, bali zitaongezwa katika mikoa mingine, hasa ile ya Pwani, kwa sababu taka, hasa za plastiki, huathiri vibaya zaidi maeneo ya baharini.

“Uchumi Rejeshi ni fursa ya kiuchumi, kiteknolojia na kimazingira. Kwa kuwekeza katika kurejesha thamani ya taka, tunalinda mazingira na wakati huo huo, tunafungua ajira za ubunifu mpya kwa vijana na jamii yetu,” amesema afisa huyo wa UNDP

Nyanda amehitimisha kwa kusisitiza kuwa uchumi rejeshi ni suluhisho la pande zote kwa Tanzania, unaolinda mazingira huku ukijenga ajira na fursa mpya za biashara.

TAGS: Tabianchi na MAzingira/AFrika/Mtwara/Tanga/Uchumi Rejeshi/UNDP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *