Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku tatu baada ya kuachishwa kazi aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Romain Folz kufuatia kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa taifa wa Bingu nchini humo Yanga imeahidi Kocha Mpya atapatikana ndani ya siku tatu.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Oktoba 21, 2025. Ofisa habari wa Klabu hiyo, Ally Kamwe amesema tayari timu imeshaingia kambini huku mchakato wa kumtafuta kocha mkuu ukiendelea.

“Kwa taarifa rasmi kutoka kwa kamati yetu tendaji inayosimamia huo mchakato, ndani ya siku tatu zijazo watakuwa wameshakamilisha huo mchakato wa kumpata kocha mpya,” amesema Kamwe huku akithibitisha kuwa katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers, Yanga itaongozwa na kocha msaidizi, Patrick Mabedi.

“Mchezo wa siku ya Jumamosi utaongozwa na kocha wetu msaidizi, Patrick Mabedi wakati mchakato wa kumtafuta kocha wetu unaendelea na ndani ya siku tatu zijazo mchakato unaweza kukamilika tukawa tumeshampata kocha wetu,” amesema Ally Kamwe katika mkutano na wana habari.

Mashabiki kuingia bure kwa Mkapa

Kuhusu mashabiki kuingia bure kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Silver Strikers utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Kamwe amesema kwamba wamepokea jumbe nyingi kutoka kwa wanachama na mashabiki wa timu yao zikielekeza ombi maalumu kwenda kwa kamati tendaji ya Yanga wakiitaka iondoe viingilio kwenye mchezo huo.

“Tumepokea jumbe mbalimbali kutoka kwa wanachama na mashabiki wetu na zote zilikuwa zinaelekeza ombi maalumu kwenda kwa kamati tendaji kuomba uongozi Yanga, mechi ya siku ya Jumamosi itolewe viingilio tuwakabidhi wao, tuifanye kuwa mechi maalumu ya mashabiki na wanachama wa Yanga kwenda kuibeba timu yao na kuipeleka hatua ya makundi.

“Asubuhi leo viongozi wamekutana wamejadili maombi hayo wamepitia hoja ambazo wanachama wamezihainisha na wamekubaliana kulipokea na wamelipitisha ombi hilo.

“Uongozi wa Yanga umekubaliana mechi hii ya Jumamosi dhidi ya Silver Strikers, mechi ya maamuzi ya kuipeleka Yanga katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa msimu huu mechi hii imeondolewa viingilio majukwaa yote, hisipokuwa jukwaa la VIP A na jukwaa la VIP B yatatumika kwa wageni watakaoarikwa.” amesema Ally Kamwe.

Aidha Ofisa habari huyo amekiri kuwa lilikuwa ombi gumu kupita lakini kwa sababu ya kipaumbele cha Klabu kwa sasa ni kufika katika hatua ya makundi viongozi wameweza kulipitisha.

Yanga itakuwa na kibarua kigumu cha kupindua meza Jumamosi Oktoba 25, 2025 baada ya kufungwa bao 1-0 ugenini nchini Malawi hivyo ili kuhakikisha inatinga hatua ya makundi inatakiwa kupata ushindi wa tofauti ya mabao mawili au zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *