
Dodoma. Serikali ya Tanzania imetangaza utekelezaji wa kubana matumizi katika magari hautahusisha yaliyopo sasa badala yake unaandaliwa mpango wa kutonunua magari ya kifahari.
Hata hivyo, mpango wa kubana matumizi kwenye magari hautakiwi kuwa kikwazo cha kusababisha upungufu wa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 28, 2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema magari yaliyokwishanunuliwa hayatauzwa kama ambavyo imekuwa ikitajwa.
Msigwa ametoa kauli hiyo alipotakiwa kujibu swali kuhusu tangazo la kubana matumizi ambalo lilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na baadaye Spika wa Bunge, Mussa Zungu ambaye naye ametangaza kuachana na magari ya kifahari.
“Katika jambo hili hatuwezi kusema tutauza magari yaliyopo sasa ila tutarekebisha kwenye sheria ya manunuzi ili tuweze kununua magari yenye unafuu.
“Lakini tukubaliane ni lazima kuhakikisha huduma hazisimami wala mpango huo usipelekee tukashindwa kuwafikia wananchi,” amesema Msigwa.
Juni 25, 2026, bungeni jijini Dodoma, Spika Zungu alisema Serikali inapaswa kuangalia matumizi ya magari kwani yamekuwa yakitafuna fedha nyingine ambazo zingeweza kutelekezwa kwenye maeneo mengine yenye tija.
Zungu akijenga hoja yake kwa takwimu halisi, alilieleza Bunge magari ya kifahari ‘mashangingi’ yanayotumiwa na viongozi wa ngazi mbalimbali yanatafuna mabilioni ya shilingi ambayo yangeweza kutumika maeneo mengine muhimu.
Si spika pekee, hata Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi alisema bungeni, kuwa eneo la matumizi ya magari serikalini inatumia fedha nyingi na ni wakati mwafaka iangaliwe upya.
Aprili 8, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi Ikulu ya Chamwino, Dodoma alisema ni umuhimu taasisi za umma kuanza kuchukua hatua za makusudi kupunguza gharama zisizo za lazima.
“Ndani ya Serikali tuna matumizi makubwa sana ya mafuta, magari ni mengi, safari zetu ni nyingi, niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta na ninaanza na ofisi yangu.
“Kuanzia sasa, ninapokwenda popote, maofisa wote nitawaingiza kwenye kibasi kimoja. Msafara utakuwa na eskoti yangu, polisi na gari ya akiba nyuma. Wanaobakia wote wataingia kwenye kibasi ili kupunguza matumizi ya mafuta,” alisema Rais Samia.
Katika mkutano wake na waandishi, Msigwa ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema tangu agizo la Rais Samia lilipotolewa, Serikali imeshatoa maelekezo kwa watumishi wa umma ambao wengi wanatumia usafiri wa kawaida.
Kuhusu kupanda kwa bei ya sukari, amesema linatokana na athari za kivita ambazo zimeongeza gharama katika usambazaji wa bidhaa ambapo bei kwa bidhaa nyingi zipo juu kwa sasa.
Ametaja kile alichoita upotoshaji kwamba baadhi ya watu hawasemi mazuri yaliyofanyika badala yake wanataka Watanzania kuamini deni la Taifa limeongezeka bila tija.
“Najua hawatawaambia kwamba tumekopa tukajenga Bwawa la Mwalimu, hawatawaambia kwamba tumekopa kwa ajili ya kujenga reli ya SGR katika vipande vitano, naomba muwaambie Watanzania kuwapuuza watu wa aina hiyo,” amesema Msigwa bila kuwataja watu hao.
Amesema kukuwa kwa deni la Taifa siyo shida kwani fedha zinazokopwa zinakuja kuharakisha maendeleo lakini mwisho wa siku lazima zilipwe.
Msigwa wamewaita Watanzania kwenye maonyesho ya biashara ya sabasaba (Tan trade) ambayo yameanza leo Juni 28 hadi Julai 13,2026.
Msimamizi wa Tantrade Kanda ya kati, Sudi Mtengela amesema mataifa 20 yamethibitisha kushiriki kwenye maonyesho hayo lakini kampuni kubwa 40 zimeshaanza maonyesho hayo.
Kwa upande wa Wizara ya Habari, Msigwa amesema wanakwenda kushiriki kongamano kubwa la Kiswahili nchi Ufaransa kuanzia Julai 4 – 7, 2026 ambalo ameeleza litakuwa na fursa nzuri kwa Watanzania.