
Katika kikao hicho kinachojikita na kuganga yajayo baada ya miaka 80 alianza kwa simulizi ya mwaka 1946 wakati karatasi ya ujumbe ulipopatikana ndani ya sanduku la kwanza la kura la Baraza. ulikuwa umeandikwa na mhandisi kutoka New York, Paul Antonio, aliyelitengeneza sanduku hilo la kupigia kura la Baraza la Usalama na kuacha ujumbe wa matumaini.
Guterres amenukuu ujumbe huo “Mungu awe pamoja na kila mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kupitia juhudi zenu tukufu, mlete amani ya kudumu kwa wote ulimwenguni.”
Katibu Mkuu amesema ujumbe huo unakumbusha lengo kuu la Baraza la Usalama ambalo ni watu.
Amesema “Heshima ya kuketi mezani hapa inakuja na wajibu zaidi ya yote wa kuheshimu imani ya watu hao. Na kuelekeza rasilimali ambazo mara nyingi hutumika kwa vita, katika maendeleo na amani.”
Katika kipindi cha miongo minane, Baraza la Usalama limeisaidia Cambodia kutoka kwenye mauaji ya halaiki, Afrika Kusini kutoka kwenye ubaguzi wa rangi, na kudumisha amani katikakatika nchi za Liberia na Timor-Leste.
Lakini Guterres ameonya kuwa uhalali wa chombo hicho sasa uko hatarini akisema“Wakati wanachama wanapotenda kinyume na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, uaminifu kwa taasisi nzima unaporomoka. Mageuzi ya Baraza la Usalama si tu muhimu lakini yamechelewa kwa muda mrefu.”
Umoja wa Mataifa na Baraza hilo wakiangalia mustakbali ametoa wito wa kuongeza uwakilishi hasa kwa bara la Afrika, Amerika ya Kusini, na ukanda wa Asia-Pasifiki na kupunguza matumizi ya kura ya turufu au veto ambayo mara nyingi huzuia hatua muhimu wakati wa migogoro.
Akihitimisha ujumbe wake, Guterres ametoa wito wa moja kwa moja kwa dhamira ya wajumbe wa Baraza. Anasema “Baraza la Usalama si kuhusu mataifa makubwa wala falme. Ni kuhusu wazazi waliopoteza watoto wao wakimbizi waliofurushwa katika makazi yao, wanajeshi waliopoteza viungo vyao. Kwa walioketi mezani hapa, nawasihi kuweni wanaostahili taji hilo la amani.”
Amesisitiza kuwa miaka 80 baadaye, ujumbe wa mhandisi Paul Antonio bado unasikika, dunia inategemea Umoja wa Mataifa kulinda amani.