Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video akiwa jijini New York Marekani katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Guterres amesema wakati wa kuundwa shirika hilo watu wote walizingatiwa na wote kupewa majukumu. “Sisi watu wa Umoja wa Mataifa…” Haya si maneno tu ya utangulizi wa Chata ya Umoja wa Mataifa ni maneno yanayotuainisha sisi ni akina nani.”

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa ni zaidi ya taasisi. “Ni ahadi inayoishi ikivuka mipaka, ikiunganisha mabara, ikihamasisha vizazi. Kwa miaka themanini, tumefanya kazi kujenga amani, kukabili umaskini na njaa, kusongesha haki za binadamu, na kujenga dunia iliyo endelevu zaidi –pamoja.”

Akiangazia siku za usoni amesema “tunavyoangalia mbele, tunakabiliwa na changamoto kubwa: mizozo inayoongezeka, zahma ya tabianchi, teknolojia za hali ya juu, na tishio la muundo wa taasisi yetu. Huu si wakati wa uoga au kurudi nyuma. Sasa, kuliko wakati wowote ule, dunia lazima ijizatiti kutatua matatizo ambayo si taifa moja linaweza kutatua peke yake. 

Akahitimisha ujumbe wake kwa kutaka ushirikiano zaidi duniani huku watu wote wakitambua Umoja wa Mataifa ni wao

“Katika siku hii ya Umoja wa Mataifa, hebu tushikamane na tukidhi ahadi yetu ya kipekee ya Umoja wenu wa Mataifa. Hebu tuoneshe dunia kile kinachowezekana pindi ‘sisi watu’ tunapoamua kuchukua hatua kwa pamoja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *