
Kahama. Wapiga kura 271, 933 waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, vyama tisa vya siasa vilivyosajiliwa katika Jimbo la Kahama Mjini mkoani Shinyanga, vinatarajiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 nchi nzima.
Vituo 669, vikiwemo 201 vya wazi vitatumika katika shughuli ya upigaji wa kura katika kata 20 za Kahama Mjini, huku makarani 669, wasimamizi 669 na wasimamizi wasaidizi 669 wakiongoza shughuli hiyo.
Msimamizi wa uchaguzi Kahama Mjini, Sadick Kigaile amesema hayo leo Oktoba 25, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi na kueleza kuwa mazingira ya vituo vyote yamezingatia wenye mahitaji maalumu.
Wakati huohuo, leo Jumamosi akifungua mafunzo kwa makarani waongozaji wa uchaguzi Kahama Mjini, Kigaile amewaonya kusimamia viapo vyao na kujiepusha kuwa chanzo cha malalamiko na vurugu wakati wote wa upigaji kura.
Amewataka kutoonyesha upendeleo wa vyama vya siasa wakati wa shughuli hiyo, ili kuufanya uchaguzi kuwa huru na haki kama ilivyo dhamira na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Amesema, “Ni vyema mkajiepusha kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa kwa kushirikiana vyema na mawakala wa vyama vya siasa, watakaokuwa kwenye vituo vyao kwa mujibu wa sheria.”
Amesema uchaguzi ni shughuli inayojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na sheria ambazo zinapaswa kufuatwa na kuzingatiwa hususani katika ngazi ya kituo ambapo shughuli hiyo hufanyika na hatimae matokeo ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Hatua na taratibu hizi ni za msingi wa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa uchaguzi,” amesema na kuongeza;
“Ninawaasa kuendelea kusoma katiba, sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya tume na msipopaelewa muhoji ili kuwarahisishia katika utekelezaji wenu wa shughuli ya uchaguzi.”
Akizungumza kwa niaba wa washiriki hao, msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Nyandekwa Manispaa ya Kahama, Damian Kilyenyi ameahidi kuzingatia sheria za INEC na maelekezo yatakayotokelewa kwenye mafunzo hayo.