Taarifa kutoka New York Marekani imemnukuu Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher akisema kuwa mapigano hayo, ambayo yamehusisha mashambulizi makubwa ya ardhini na makombora, yameigeuza El Fasher kuwa uwanja wa vita unaohatarisha maisha ya maelfu ya watu.

Fletcher amesema “Wapiganaji wanazidi kusogea ndani ya mji, njia za kutoroka zimefungwa, na mamia ya maelfu ya raia wamekwama wakiwa na hofu kubwa, wakishambuliwa, wakiwa na njaa na bila huduma za afya wala maeneo salama,”

Amesisitiza kuwa ni lazima kuruhusu upatikanaji wa haraka, salama na usiokatizwa wa misaada ya kibinadamu kwa raia wote wanaohitaji msaada. “Tunazo bidhaa za kuokoa maisha tayari, lakini mashambulizi yanayoendelea yamefanya isiwezekane kufikisha misaada. Wafanyakazi wa mashirika ya ndani wanaendelea kuokoa maisha wakiwa chini ya mashambulizi.”

Wito wa kusitishwa mapigano

Fletcher ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano mjini El Fasher, katika eneo lote la Darfur na nchini Sudan kwa ujumla. Amesema raia lazima waruhusiwe kutafuta usalama kwa heshima na bila vitisho, na wale wanaobaki wakiwemo wahudumu wa kibinadamu walindwe ipasavyo.

“Shambulio lolote dhidi ya raia, hospitali au shughuli za kibinadamu lazima likome mara moja,” amesema mkuu huyo wa OCHA

Pia amesisitiza kuwa wote wanaohusika na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu lazima wawajibishwe, akiwakumbusha wahusika wote wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2736 (2024).

Taarifa hii inakuja wakati mapigano yanazidi kuongezeka nchini Sudan, yakisababisha maelfu ya vifo, uharibifu mkubwa wa miundombinu na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu kote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *