Msemaji wa OHCHR, Seif Magango, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya video kutoka Nairobi, Kenya amesema ofisi hiyo imepokea taarifa za kuaminika zikionesha kuwa watu wasiopungua 10 wameuawa katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Morogoro, kufuatia hatua za vyombo vya usalama kutumia risasi na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Magango amesema kuwa marufuku ya kutotoka nje imewekwa kote nchini, huku mtandao wa intaneti ukiwa umepunguzwa kwa kiwango kikubwa tangu kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, bila sababu rasmi kutolewa na mamlaka.

“Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi au yasiyo ya lazima, ikiwemo silaha za moto, dhidi ya waandamanaji, na badala yake kufanya kila juhudi kupunguza mvutano uliopo. Waandamanaji nao wanapaswa kuonyesha nia ya amani katika maandamano yao,” amesema Magango.

OHCHR pia imeitaka serikali ya Tanzania kuzingatia wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kurejesha huduma ya intaneti mara moja na kuhakikisha wananchi wanatimiza haki zao za uhuru wa kujieleza, kushirikiana na kukusanyika kwa amani.

“Kukandamiza mawasiliano kutazidisha kukosekana kwa imani ya umma katika mchakato wa uchaguzi,” ameongeza msemaji huyo.

Magango amebainisha kuwa vurugu hizo za baada ya uchaguzi zinakuja baada ya kampeni zilizogubikwa na madai ya kukamatwa kiholela kwa viongozi wa upinzani, wakiwemo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, na naibu wake, pamoja na taarifa za watu kutoweka kwa lazima, akiwemo balozi wa zamani wa Tanzania nchini Cuba.

OHCHR imesisitiza kwamba watu wote waliokamatwa kiholela wanapaswa kuachiliwa mara moja bila masharti, na wale wanaoshikiliwa kwa mujibu wa sheria wapewe haki kamili za mchakato wa haki na kesi ya haki.

Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa mamlaka nchini kuhakikisha uchunguzi wa haraka, huru na wa kina unafanyika kuhusu visa vyote vya vurugu vinavyohusiana na uchaguzi, na kwamba wote waliohusika na ukiukwaji wa haki wanachukuliwa hatua za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *