Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon Hizbullah Sheikh Naim Qassem, amesisitiza kuwa Hizbullah haitasalimu amri kwa vitisho vya Marekani kwa sababu nchi hiyo si mpatanishi asiyeegemea upande wowote na inaunga mkono utawala wa Kizayuni na uvamizi wa Israel.

Akizungumzia madai ya Marekani ya kufanya mageuzi nchini Lebanon, Sheikh Naim Qassem amesema: Marekani inadai inataka kutatua matatizo ya Lebanon, lakini si mpatanishi asiyeegemea upande wowote, bali ni msaidizi na muungaji mkono wa wavamizi. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa: “Wakati wowote inapotangazwa kwamba mjumbe wa Marekani atafanya safari katika eneo hili, uchokozi wa utawala wa Kizayuni pia huongezeka na mashinikizo hushtadi.”

Wakati huo huo, “Mohammed Al-Ra’ad,” Mkuu wa kundi la Loyalty to the Resistance katika Bunge la Lebanon, pia amesema: “Kukubali kulegeza kamba kwa adui au kuhalalisha visingizio vyake vya kichokozi hakutauzuia utawala wa Kizayuni kutaka kujitanua zaidi na kutauhamasisha kuibua madai ya kukalia kwa mabavu ardhi yetu yote.”

Mohammed Al-Ra’ad

Katika hali ambayo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinataka kudhoofisha mhimili wa Muqawama nchini Lebanon kupitia mipango ya kisiasa na kiusalama, kusimama kidete kwa Hizbullah na harakati za Muqawama si tu kwamba ni jibu la kujihami bali pia ni mkakati wa kitaifa na kikanda wa kulinda uhuru, kujitawala na usalama wa Lebanon. Kupitia njia ya kuishinikiza serikali ya Lebanon ili iipokonye silaha harakati ya Hizbullah, Marekani inafanya njama za kufutulia mbali nguvu yenye taathira na ya kujilinda ambayo imezuia uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Lebanon na eneo zima la Magharibi mwa Asia. Hivyo basi, kusimama imara Muqawama wa Lebanon dhidi ya njama za pamoja za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kunadhamini usalama wa kikanda, uhuru, kujitawala na utulivu, na kuzuia mipango na njama za kufanikisha malengo yao ya kujipanua na ya kivamizi. Muqawama wa Lebanon, hasa Hizbullah, umekuwa na mchango muhimu katika kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni.

Marekani inajionyesha kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote, lakini kivitendo, inafanya mikakati ya kudhoofisha Muqawama na kubadilisha milinganyo ya nguvu katika eneo la Asia Magharibi kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kuishinikiza serikali ya Lebanon ili itekeleze mipango kama ule wa “kuwekwa silaha zote mikononi mwa serikali.” Njama hii ya pamoja ya Wamarekani na Wazayuni ya kutaka kuipokonya silaha Hizbullah inaifanya Lebanon iwe katika hatari ya vitisho vya nje na kuhatarisha usalama wa ndani wa nchi hiyo.

Inatupasa pia kusema kuwa, kulegeza kamba kwa aina yoyote mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel si tu kwamba hakutazuia uchokozi wa utawala huo, bali pia kutauhamasisha zaidi kutoa madai mengine, ikiwa ni pamoja na kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi yote ya Lebanon.

Muqawama wa Lebanon, ukiongozwa na Hizbullah, umekuwa na mchango muhimu katika kukabiliana na mipango ya kujitanua ya utawala wa Kizayuni. Kusimama kidete Muqawama wa Lebanon dhidi ya njama za Marekani na utawala wa Kizayuni si tu kwamba ni dharura ya kujilinda bali pia ni mkakati mwerevu wa kudumisha uhuru, usalama, na utulivu wa kikanda. Muqawama huu ni kikwazo kwa malengo ya kutaka kujitanua ya kutawala wa Kizayuni ambayo yanafuatiliwa kwa kauli mbiu ya udanganyifu na madai ya upatanishi.

Vilevile inatupasa kuelewa kwamba, kusimama kidete Hizbullah kunatambuliwa kuwa ni mfano na kigezo cha kuigwa na nchi zingine katika eneo la Magharibi mwa Asia dhidi ya mashinikizo ya nje na njama za pamoja za Magharibi na Uzayuni. Harakati ya Hizbullah sio tu kwamba inaungwa mkono sana na watu, bali pia ina nafasi muhimu katika muundo wa kisiasa wa Lebanon. Uungaji mkono huu ni nguzo muhimu sana ya kuendeleza njia ya Muqawama dhidi ya mashinikizo ya kigeni.

Itakumbukwa kuwa, baada ya operesheni ya kihistoria ya “Kimbunga cha Al-Aqsa” mnamo Oktoba 7, 2023, Muqawama wa Lebanon, haswa Hizbullah, ulikuwa na nafasi kubwa katika kutetea kambi ya Muqawama wa Palestina. Utendaji huu ulikuwa na athari kubwa kwa matukio ya kikanda katika ngazi zote za kijeshi, kisiasa na kisaikolojia.

Kimbunga cha al Aqsa 

Utendaji wa Hizbullah baada ya Kimbunga cha Al-Aqsa uliimarisha mshikamano miongoni mwa makundi ya Muqawama nchini Lebanon, Palestina, Iraq, na Yemen. Mshikamano huo ulituma ujumbe wazi kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba uchokkozi wowote wa utawala wa Kizayuni utapata majibu mwafaka kutoka kwa makundi ya Muqawama katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *