Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed al-Sudani alisema jana Jumatatu kwamba kuondoka kikamilifu Marekani na muungano wake unaodaiwa wa kupambana na Daesh huko Iraq ndiko kutakakopelekea kupokonywa silaha makundi ya kujihami ya wananchi. Kwa mujibu wa makubaliano, Marekani lazima iondoke Iraq mwezi Septemba mwaka ujao wa 2026.

Waziri Mkuu wa Iraq amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters mjini Baghad na kujibu swali akisema: “Daesh (ISIS) hawapo tena. Kuna usalama na utulivu Iraq hivi sasa, namshukuru Mungu … Kwa hivyo ni nini sababu ya nchi 86 kuendelea kuwepo Iraq kwa mwavuli wa muungano wa kupambana na ISIS?” 

Amesema: “Baada ya kuondoka Marekani kwa hakika kutakuwa na mpango wa wazi wa kuyapokonya silaha makundi ya kujihami ya wananchi. Hicho ni kitu ambacho kinakubaliwa na watu wote wa Iraq.”

Aidha ameeleza kwamba vikundi vya kujihami vya wananchi vinaweza kukabidhi silaha zao na kujiunga na vikosi rasmi vya usalama au kuingia katika siasa baada ya kuondoka Marekani mwezi Septemba 2026.

Marekani na Iraq zimekubaliana kuhusu kuondoka wanajeshi wa Marekani kwa awamu. Wamarekani wanatarajiwa kuondoka kikamilifu Iraq ifikapo mwezi Septemba 2026. Wanajeshi wa Marekani wameanza  kupunguzwa nchini Iraq mwaka huu wa 2025.

Akigusia shughuli za makundi ya kujihami ya wananchi nchini Iraq, Al-Sudani amesema: “Sheria ziko wazi katika nafasi zake za kudumisha usalama na utulivu na kwamba taasisi za serikali ndizo zinazofanya maamuzi katika nyakati za vita na amani, na hakuna upande wowote unaoweza kuiingiza Iraq katika vita au migogoro.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *