Rais Samia aapishwa kuiongoza tena TanzaniaRais Samia aapishwa kuiongoza tena Tanzania
Ruka sehemu inayofuata Je, hotuba ya Rais Samia ilizungumzia taarifa ya vifo vya mamia ya watu?

3 Novemba 2025

Je, hotuba ya Rais Samia ilizungumzia taarifa ya vifo vya mamia ya watu?

Tanzania Namanga 2025 | Vifo vya waandamanaji
Polisi ikiuvuta mwili wa mwandamanaji aliyeuawa katika eneo la Namanga jijini Dar es Salaam wakati wa maandamano ya siku ya uchaguzi mkuu uligubikwa na vurugu nchini Tanzania.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Licha ya taarifa za vifo vilivyotokea wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi, hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa baada ya kuapishwa haikugusia suala hilo. 

Kiongozi huyo hata hivyo, alizungumzia kidogo kile alichokiita “vitendo vya uvunjifu wa amani” vilivyosababisha hasara ya “vifo na uharibifu wa mali” na kuelezea masikitiko yake bila kutaja idadi ya waliopoteza maisha au kile kilichosabisha vifo hivyo.  

Ijumaa wiki iliyopita, Chama cha upinzani cha CHADEMA kilisema watu wasiopungua 700 waliuawa katika siku tatu za baada ya uchaguzi. Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International, lilisema limepokea taarifa ya vifo visivyopungua 100. Serikali ya Tanzania ilikanusha taarifa hizo bila kutoa maelezo ya kile inachofahamu.

Tangu jana Jumapili, mitandao ya kijamii nchini Tanzania imefurika picha na video zinazoonesha watu miili ya makumi ya watu na wengine waliojeruhiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa risasi za polisi. DW Kiswahili inaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa hizo ili kupata ushahidi usio na mashaka. 

https://p.dw.com/p/531Y4

Ruka sehemu inayofuata Serikali Tanzania yasema shughuli za kawaida kurejea Jumanne

3 Novemba 2025

Serikali Tanzania yasema shughuli za kawaida kurejea Jumanne

Msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa
Msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa.Picha: Privat

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amearifu kupitia mitandao ya kijamii kuwa shughuli za kawaida zitarejea Jumanne ya Novemba 04, 2025. 

“Kama alivyoelekeza Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hotuba yake baada ya kuapishwa, kesho Jumanne… wananchi wote wanajulishwa kurejea kwenye shughuli zao za kila siku za kiuchumi na kijamii”, imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Msigwa. 

Sehemu kubwa za shughuli za kawaida chini humo zilisimama tangu uchaguzi wa Oktoba 29, kutokana na maandamano makubwa ya umma ya kuupinga uchaguzi. Polisi pia ilitoa amri ya kutotoka nje baada ya saa kumi na mbili jioni kwa lengo la kile ilisema “kudhibiti makundi ya watu yanayosababisha fujo”.

Miji mikubwa kama Dar es Salaam, maandamano ya umma yalikumbwa na vurugu ikiwemo vitendo vya uchomaji moto mali, uporaji maduka na makabiliano kati ya polisi na wananchi. Upinzani unasema vurugu hizo zimesababisha vifo vya mamia ya waandamanaji. Serikali hadi sasa haitoa taarifa kuhusu idadi ya vifo wala majeruhi.  ambayo  pia vurugu 

https://p.dw.com/p/531HL

Ruka sehemu inayofuata Huduma ya Intaneti yarejea Tanzania

3 Novemba 2025

Huduma ya Intaneti yarejea Tanzania

Picha ikionesha APPS maarufu za mitandao ya kijamii
Kwa karibu siku tano, huduma ya mtandao wa intaneti haikuwa ikipatikana nchini Tanzania baada ya mamlaka nchini humo kuzifunga kwa madai ya “kuzuia uchochezi wa machafuko”.Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Taarifa kutoka nchini Tanzania zinasema huduma ya mawasiliano kwa njia ya intaneti zimerejea karibu siku tano tangu zilipopotea hewani. Mwenzetu Sudi Mnette aliyepiga kambi nchini Tanzania kwa ajili ya uchaguzi amethibitisha taarifa hizo na kwamba sasa anaweza tena kutuma bila usumbufu taarifa kutoka nchini humo. 

DW Kiswahili imewasiliana pia na mwandishi wa habari nchini Tanzania Martin Nyoni. “Ndio tumerejea hewani taratibu”, ameandika Nyoni kupitia mtandao wa WhatsApp ambao tangu Alhamisi ya Oktoba 30 haukuwa ukipatikana nchini Tanzania. 

“Ilikuwa shida sana kila kitu, kililala …unaandaa ripoti yako lakini mwisho wa siku huezi kuituma popote pale”, ameongeza kusema Nyoni, ambaye tangu siku ya uchaguzi alikuwa amekita kambi Dodoma kwa lengo la kuandaa ripoti kwa ajili ya kituo kimoja cha redio anachofanyia kazi kaskazini mwa Tanzania. 

https://p.dw.com/p/5319S

Ruka sehemu inayofuata ´Kiza cha Intaneti´ bado chaigubika Tanzania

3 Novemba 2025

´Kiza cha Intaneti´ bado chaigubika Tanzania

Raia nchini Tanzania bado wanaishi kwenye ´kiza totoro cha intaneti´ tangu huduma hiyo muhimu ilipokatwa karibu siku tano zilizopita kwa sababu ya kile mamlaka zimesima “kuzima wimbi la vurugu zilizokuwa zinachochewa mtandaoni”

Biashara za mtandaoni zimesimama, huduma ya mawasiliano kwa njia hiyo hazipatikani na Watanzania walio wengi hawaonekani Istagram, Facebook wala Twitter. 

Inaarifiwa hata njia ya kutumia teknolojia ya kukwepa kizuizi “virtual private network” au kwa kifupi VPN pia haifanyi kazi kwa sababu mawasiliano ya mtandao yamezimwa. 

Watanzania waliozungumza na DW Kiswahili wamelalamikia hali hiyo. Tizama video hii kwenye ukurasa wetu wa Instagram:  Kilio cha intaneti Tanzania

https://p.dw.com/p/530o7

Ruka sehemu inayofuata SADC: Uchaguzi Tanzania ulipungukiwa sifa za demokrasia

3 Novemba 2025

SADC: Uchaguzi Tanzania ulipungukiwa sifa za demokrasia

Ripoti ya awali ya waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema uchaguzi uliofanyika Tanzania ulipungukiwa sifa na misingi inayokubalika ya kidemokrasia.

Ujumbe wa waangalizi ulioongozwa na Richard Msowoya wa Malawi umesema “kwenye maeneo mengi, wapiga kura hawakupata nafasi ya kutekeleza takwa lao la kidemokrasia” la kuchagua viongozi. 

Ujumbe huo pia umesema, kwa ujumla uchaguzi wa Tanzania haukuwa na sifa zote zinazokubalika na SADC kama msingi wa chaguzi za kidemokrasia.

Ripoti yao imegusia pia kukosekana kwa huduma ya intaneti kama kizingiti kikubwa kilichotatiza mawasiliano baina ya waangalizi na haki ya wananchi kupata taarifa. kwenye ripoti hiyo kuwa miongoni mwa vikwazo vilivyouzonga uchaguzi huo wa Oktoba 29. 

Vurugu zazuka Namanga kufuatia Uchaguzi wa utata Tanzania

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

https://p.dw.com/p/530Xa

Ruka sehemu inayofuata Museveni wa Uganda ampongeza Samia

3 Novemba 2025

Museveni wa Uganda ampongeza Samia

Viongozi kadhaa wa Afrika wamemtumia salamu za pongezi Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kufuatia kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 29.

Tayari marais wa Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi na Burundi walikwishatuma salamu za pongezi. 

Rais Yoweri Museveni wa Uganda naye amejiunga na wengine kumpongeza Rais Samia. Amesema ushindi wake “unaakisi imani ya Watanzania katika uongozi na maono yake:”

Museveni pia amesema yuko tayarikuendelea kufanya kazi na kiongozi huyo wa Tanzania ili kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili jirani. 

https://p.dw.com/p/530bx

Ruka sehemu inayofuata Je, Samia atafanikiwa kuiunganisha Tanzania baada ya uchaguzi?

3 Novemba 2025

Je, Samia atafanikiwa kuiunganisha Tanzania baada ya uchaguzi?

Wakati wa hotuba yake baada ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amesema atafanya kazi ya kuliunganisha taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo kwa kipimo chochote kile ni kwa hakika limegawika baada ya uchaguzi.

Chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimeyapinga matokeo yaliyompa ushindi Samia na maelfu ya watu waliingia mitaani kuupinga uchaguzi. 

Je, kiongozi huyo atafaulu kuliunganisha taifa hilo? Tizama video hii: 
 

Ghasia za baada ya uchaguzi Tanzania,Mtihani kwa rais Samia

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

https://p.dw.com/p/530Z1

Ruka sehemu inayofuata Rais Samia: Nitafanya kazi ya kuunganisha taifa

3 Novemba 2025

Rais Samia: Nitafanya kazi ya kuunganisha taifa

Rais Samia na Tundu Lissu
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu mnamo Februari 16, 2022 mjini Brussels, Ubelgiji. Mkutano huo ulikuwa sehemu ya hatua za mwanzo za maridhiano ya kisiasa yaliyoanzishwa na Rais Samia.Picha: Sudi Mnette/Mohammed Khelef/DW

Sehemu ya hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan imegusia haja ya kufanya maridhiano.

Kiongozi huyo amesema ataendelea na juhudi alizoanzisha za kusaka maridhiano na mageuzi chini ya falsafa yake ya “4Rs”. Falsafa hii inajikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding). 

“Niwasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya vinyongo, umoja badala ya mgawanyiko na amani badala ya vurugu”, amesema Samia.

Wito wa maridhiano umetolewa pia na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia ambaye tayari tulikuarifu hapo kabla. 
 

https://p.dw.com/p/530NK

Ruka sehemu inayofuata Samia azungumzia athari za maandamano

3 Novemba 2025

Samia azungumzia athari za maandamano

Tanzania Namanga 2025 | Polisi ikishika doria nchini Tanzania
Mashirika kadhaa ya haki za binadamu yamesema vurugu za wakati wa uchaguzi nchini Tanzania zimesababisha vifo vya makumi au mamia ya watu.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Sehemu ya hotuba ya Rais wa Tanzania pia imegusia wimbi la maandamano ya umma   lililogubika nchi hiyo siku ya uchaguzi na siku mbili baada ya uchaguzi.

Amesema, yeye na “wote tunaoitakia mema nchi hii, tumesikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali…hasa kwenye majiji na miji”. 

Amesema kilichotokea hakiendani na “sifa na taswira ya Kitanzania” na kwamba siyo “Utanzania”. Kiongozi huyo pia amedai kuwa baadhi ya vijana waliokamatwa kwenye wimbi hilo la maandamano ya umma walitoka nje ya Tanzania.

Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo hadi sasa haijatoa maelezo ya kina wala ushahidi wa taarifa hizo. Vilivile Samia, amesema hivi sasa vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo vinafanya kazi ili kurejesha utulivu. 

https://p.dw.com/p/5309C

Ruka sehemu inayofuata Rais Samia: Uchaguzi umekwisha, tuanze kazi

3 Novemba 2025

Rais Samia: Uchaguzi umekwisha, tuanze kazi

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru wanasiasa walioshiriki uchaguzi ikiwemo wagombea wengine 16 waliowania kiti cha urais.

Amesema wanasiasa hao wametambua kuwa “uchaguzi sio vita”. Kiongozi huyo pia amewapongeza wale waliochaguliwa kushika nafasi za ubunge na udiwani kote nchini humo na kuwahimiza kujielekeza kuchapa kazi kwa ajili ya raia wa taifa hilo.
 

https://p.dw.com/p/5305o

Ruka sehemu inayofuata Rais Hichilema: Rais Samia wanyooshee wapinzani mkono wa mapatano

3 Novemba 2025

Rais Hichilema: Rais Samia wanyooshee wapinzani mkono wa mapatano

Katika hotuba yake, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amemtolea mwito Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kunyoosha mkono wa mapatano na upinzani na wale wanaopinga utawala wake au hakumchagua katika uchaguzi uliomalizika.

Amesema Zambia inamtakia kila la kheri anapoanza muhula mpya wa uongozi na amewarai Watanzania kuendelea kuwa watulivu na kulinda amani. 

Hichilema pia amesema; “Raia wa Zambia wako pamoja nanyi, tunaelewa changamoto (na) maumivu yenu, pamoja na fursa mlizo nazo, ambazo ni nyingi. Chukueni upande wa fursa (zilizopo) na kila kitu kitakuwa sawa siku zijazo. Kumbukeni, wakati wa Mungu, ndio wakati sahihi.” 
 

https://p.dw.com/p/5303r

Ruka sehemu inayofuata Rais Ndayishimiye wa Burundi atoa salamu za pongezi

3 Novemba 2025

Rais Ndayishimiye wa Burundi atoa salamu za pongezi

Rais Evarist Ndayishimiye wa Burundi.
Rais Evarist Ndayishimiye wa Burundi.Picha: Tchandrou Nitanga/AFP/Getty Images

Kama tulivyokuarifu, viongozi kadhaa wa Afrika wanahudhuria sherehe za kuapishwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania kwa mara nyingine. 

Miongoni mwa waliopewa nafasi ya kuzungumza ni Rais Evarist Ndayishimiye wa Burundi. Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Tanzania kwa kumaliza uchaguzi. 

Amesema; “Ningependa kuwapongeza ninyi raia wote wa Tanzania kwa namna mlivyopiga kura… katika ulimwengu wa leo, kwa wananchi, upigaji kura ni kama mtihani, mmefaulu mtihani, hongereni sana… Amani haina bei na watanzania mmeelewa vizuri msemo huo.”

Ikumbukwe uchaguzi wa Tanzania wa Oktoba 29 ulikumbwa na vurugu na chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA kimeyapinga matokeo yake. Kuna ripoti pia za vikosi wa usalama kutumia nguvu iliyosababisha vifo vya mamia ya waandamanaji. 
 

https://p.dw.com/p/5300u

Ruka sehemu inayofuata Kiapo cha Rais wa Tanzania kinasemaje?

3 Novemba 2025

Kiapo cha Rais wa Tanzania kinasemaje?

Kula kiapo cha kuchukua nafasi ya uongozi wa juu wa nchi ni utamaduni wa kawaida kote ulimwenguni, ingawa maudhui na maneno ya kiapo hutofautiana. 

Kwa Tanzania, kiapo cha Rais kina sehemu tatu na zote hizo husomwa mtu anayeapishwa kuchukua wadhifa huo mbele ya Jaji Mkuu wa nchi hiyo.

Hii leo kiongozi huyo wa Tanzania alisema: “Mimi Samia Suluhu Hassan naapa kwamba, nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuitumikia kwa moyo wangu wote, na kwamba nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.”

https://p.dw.com/p/52zy5

Ruka sehemu inayofuata Viongozi gani wanahudhuria sherehe hizo?

3 Novemba 2025

Viongozi gani wanahudhuria sherehe hizo?

Viongozi kadhaa wa Afrika wanahudhuria sherehe za kuapishwa Samia Suluhu Hassan. Miongoni mwao ni Rais Daniel Chapo wa Msumbiji, Hakainde Hichilema wa Zambia na Evarist Ndayishimiye wa Burundi. 

Wengine ni Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki na wawakilishi wa Uganda, Zimbabwe na visiwa vya Comoro. Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi ambaye aliapishwa Jumamosi iliyopita baada ya kushinda uchaguzi naye anahudhuria sherehe hizo. 

https://p.dw.com/p/52zsa

Ruka sehemu inayofuata Samia Suluhu Hassan ni nani?

3 Novemba 2025

Samia Suluhu Hassan ni nani?

Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Tanzania mnamo Machi, 19, 2021
Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Tanzania mnamo Machi, 19, 2021. Picha: Stringer/REUTERS

Wakati sherehe za kuapishwa Samia Suluhu Hassan zinaendelea huko Dodoma, Tanzania chukua muda kumfahamu mwanasiasa huyo.

Rais Samia ambae ni mama wa watoto wanne, mzaliwa wa Zanzibar, na mwanasiasa aliyeingia kwenye ulingo wa siasa akitokea makundi ya asasi za kijamii. Samia Suluhu Hassan alishika nafasi ya urais mnamo mwezi Machi 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, ambaye alihudumu kama makamu wake kwa kipindi cha miaka mitano ya awali.

Mwenyekiti huyo wa chama kinachotawala, CCM, ana umri wa miaka 65 akiwa amesomea uchumi katika ngazi ya shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.

Soma zaidi wasifu wa kiongozi huyo: Aliyekuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Tanzania.
 

https://p.dw.com/p/52ziF

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *