Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV , ameizungumzia hali inayoendelea nchini Tanzania hivi leo Jumapili kwa kutowa mwito kwa pande zote kujiepusha na machafuko na badala yake kufuata njia ya mazungumzo.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imetumbukia katika hali mbaya ya vurugu za kisiasa zilizosababishwa na uchaguzi uliopingwa na umma wa Watanzania.

Vurugu za maandamano ya kupinga uchaguzi
Vurugu za maandamano ya kupinga uchaguziPicha: AP Photo/picture alliance

Chama kikuu cha upinzani  CHADEMA  kinaamini mamia ya watu wameuwawa huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikisema ina taarifa za kuaminika zinazoonesha watu kiasi 10 wameuwawa katika miji mitatu nchini humo.

Papa Leo ameizungumzia pia hali ya Sudan

Ama kiongozi mkuu wa Kanisa katoliki duniani Papa Leo ametowa mwito pia wa kusitishwa mara moja kwa vita nchini Sudan na kufunguliwa kwa njia za kupitisha msaada wa kiutu.

Papa Leo amesema, amekuwa akifuatilia kwa masikito makubwa ripoti zinazoonesha ukatili wa hali ya juu unaofanyika katika mji wa Al Fashir katika jimbo la Darfur.

Katika hotuba yake kwa waumini ya kila wiki kwenye sala ya Jumapili katika uwanja wa  kanisa la mtakatifu Petro, huko Vatican Papa Leo ametaja juu ya mashambulizi ya kiholela dhidi ya wanawake na watoto na raia wasiokuwa na hatia kwa ujumla wake akisema ni hujuma inayozuia hatua ya kutowa msaada na kusababisha mateso yasiyokubalika.

Kikosi cha wanamgambo wa RSF wakidhibiti mji wa El-Fasher - Darfur
Kikosi cha wanamgambo wa RSF wakidhibiti mji wa El-Fasher – DarfurPicha: Rapid Support Forces/AFP

Kadhalika ameitaka jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua thabiti kusaidia juhudi za kutowa msaada.

Ofisi ya haki za binadamu ya  UN siku ya Ijumaa ilisema mamia ya raia na wapiganaji wasiokuwa na silaha huenda wameuwawa mwishoni mwa mwezi Oktoba baada ya wanamgambo wa RSF kuuteka mji wa Al Fashir uliokuwa ngome ya mwisho ya wanajeshi wa serikali katika jimbo la Darfur.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *