Dar es Salaam. Serikali imetangaza kusitisha usafiri wa mabasi ya yaendayo haraka maarufu mwendokasi jijini Dar es Salaam ambazo huduma huduma kati ya Gerezani – Kimara na Gerezani – Mbagala.

Kusitishwa kwa huduma hiyo, kunalenga kutoa nafasi ya kufanyika kwa tathmini ili kujua uharibifu uliofanyika wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.

Katika maandamano hayo, waandamaji waliharibu miundombinu hususan vituo vya mwendokasi hususan vituo vilivyopo barabara ya Morogoro kwa kuvunja vituo, mifumo ya ukataji tiketi na kuvichoma moto baadhi ya vituo.

Tangazo la kusitishwa kwa huduma hiyo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Chalamila amewataka waliokuwa watumiaji wa usafiri huo kutafuta njia mbadala za usafiri wakati ambao unafanyika utaratibu wa kurudisha hali kama ilivyokuwa awali.

“Tunasitisha mara moja usafiri huu ili kufanya tathmini ya kina ya uharibifu uliotokea kwani mifumo ya ukataji tiketi imeharibiwa jambo ambalo linahitaji muda ili kurudisha hali kama ilivyokuwa awali,” amesema Chalamila na kuongeza:

“Ninawaagiza Latra (Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini) kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya kawaida ili yaweze kutoa huduma kwa njia ambazoi zilikuwa zikitegemea mabasi ya mwendokasi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *