Prague, Czech. Rekodi nne ziliwekwa na Arsenal usiku wa juzi wakati ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Slavia Prague katika Uwanja wa Fortuna Arena kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Rekodi mbili kati ya hizo ziliwekwa na Arsenal kama timu huku nyingine mbili zikiwekwa na wachezaji wake wawili tofauti.
Ushindi wa juzi umeifanya Arsenal iweke rekodi ya kucheza mechi nane mfululizo za mashindano tofauti bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa ambayo ni idadi kubwa zaidi ya mechi kuwahi kuchezwa na timu moja bila nyavu zake kuguswa.
Arsenal inashikilia rekodi hiyo sambamba na Preston iliyofanya kuanzia Januari hadi Septemba 1889 na Liverpool kuanzia Januari hadi Februari 1920.
Rekodi nyingine ambayo Arsenal imeweka ni kushinda mechi 10 mfululizo katika mashindano yote kwa mara ya kwanza chini ya Mikel Arteta ambapo mara ya mwisho ilifanya hivyo kati ya Agosti na Oktoba 2018 chini ya Unai Emery (aliyeshinda mechi 11 mfululizo).
Max Dowman wa Arsenal, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kucheza katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa hajatimiza miaka 18 ambapo juzi aliichezea Arsenal akiwa na umri wa miaka 15 na siku 308.
Naye Bukayo Saka amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Arsenal kufunga bao katika mechi nne mfululizo za ugenini za Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo katika mchezo wa juzi alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti.
Katika mchezo huo wa juzi, mabao mengine mawili ya Arsenal yalipachikwa na Mikel Merino.