
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amesema mkutano huo umeashiria “mwelekeo mpya wa makusudi” kutoka kujadili changamoto hadi kutekeleza suluhisho zilizothibitishwa. “Kama tulivyojifunza mjini Copenhagen miaka 30 iliyopita, maendeleo ya kijamii ni msingi wa jamii imara. Huu si wema wa hiari, bali ni maslahi ya kila taifa,” alisema.
Baerbock pia alionya kuwa njaa na umaskini havisababishwi na uhaba wa rasilimali, bali na migogoro, ukosefu wa usawa na kushindwa kwa kisiasa, akisisitiza kuwa tatizo si fedha, bali jinsi zinavyowekezwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya viongozi 40 wa nchi na serikali, mawaziri na maafisa wakuu zaidi ya 230, pamoja na washiriki wapatao 14,000. Zaidi ya vikao 250 vya suluhisho vilifanyika, vikilenga mbinu za vitendo za kupanua ulinzi wa kijamii, kuboresha huduma za afya na elimu, na kukuza kazi zenye heshima.
Watu wanatarajia matokeo
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, amesema matokeo ya mkutano huo yanadhihirisha shauku kubwa ya jamii, mashirika ya kiraia, vyama vya wafanyakazi, vijana na sekta binafsi kuona hatua za kweli. “Watu wanatarajia majibu, siyo maneno. Tamko la Kisiasa la Doha si nyaraka za kuwekwa kwenye makabati, bali ni ahadi ya kuweka watu katikati ya maendeleo endelevu,” alisema.
Bi. Mohammed alisisitiza kuwa utekelezaji sasa lazima ulenge kupunguza umaskini, kuongeza ajira zenye maana na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma. “Tumefungua mlango hapa Doha,” alisema, “sasa ni jukumu letu kuupita pamoja.”
Tume mbalimbali za kiuchumi nazo zilizungumza katika mkutano huo. Tume ya Uchumi ya Afrika ilisisitiza “uwezo wa vijana” wa bara hilo, ikitoa wito wa uwekezaji katika elimu, ujuzi, fursa za ajira na ujasiriamali, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika na taasisi za kikanda.