
Afrika Kusini imesema kuwa, raia wake 17 waliojiunga na makundi ya mamluki katika vita vya Russia na Ukraine wameomba msaada wa kuokolewa kutoka kwenye eneo la Donbas ambako mapigano yanaendelea.
Raia hao wanaume wa Afrika Kusini wana umri wa kati ya miaka 20 na 39. Inadaiwa kuwa waliingia kwenye mtego wa tamaa ya kupata malipo mazuri kama watashiriki kwenye vita huko Ukraine. Msemaji wa Serikali ya Afrika Kusini Vincent Magwenya amesema hayo na kuongeza kuwa, Rais Cyril Ramaphosa ameamuru uchunguzi ufanyike kuhusu jinsi watu hao walivyotumbukia kwenye kazi ambazo zinaonekana wazi ni za mamluki.
Bado haijajulikana watu hao walikodiwa kupigana kwa ajili ya upande gani wa mgogoro wa Ukraine. Sheria ya Afrika Kusini inawakataza raia wake kupigana kwa ajili ya jeshi au kundi lolote la kigeni bila ya idhini ya Serikali.
Magwenya amesema kuwa, 16 kati ya watu hao wanatoka KwaZulu-Natal na mmoja anatoka Eastern Cape. Ameongeza kuwa Pretoria inatumia njia za kidiplomasia kujaribu kuwarudisha nyumbani watu hao na kuyalaumu magenge ya magendo ya binadamu yanayowalaghai na kuwanyonya vijana walioko katika mazingira magumu.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana umewafanya raia wa Afrika Kusini kuwa shabaha rahisi ya magenge ya magendo ya binadamu.
Mwezi Agosti mwaka huu, Afrika Kusini iliwaonya raia wake hasa vijana wa kike wasiingie kwenye mitengo ya ofa bandia za kazi zilizoenea mitandaoni. Ripoti zinasema kuwa kesi kama hizo zimeemea sana katika nchi za Kenya na Nigeria.