
Utafiti mpya uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu UNODC umeonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kilimo cha mmea wa afyuni (Opium) nchini Afghanistan katika mwaka huu wa 2025, hali inayoashiria mabadiliko makubwa katika uzalishaji na biashara ya mihadarati katika ukanda huo.
Taarifa kutoka mjini Kabul, Afghanistan na Vienna, Austria imeeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti huo eneo lililotumika kulima afyuni mwaka huu linakadiriwa kufikia hekta 10,200, likiwa ni punguo la asilimia 20 ikilinganishwa na hekta 12,800 zilizoripotiwa mwaka 2024.
Takwimu hizo ni sehemu ndogo sana ya viwango vya kabla ya kilimo hicho kupigwa marufuku mwaka 2022, ambapo takribani hekta 232,000 zilikuwa zikilimwa nchi nzima.
Mwakilishi wa Kanda wa UNODC katika nchi za Afghanistan, Asia ya Kati, Iran na Pakistan Oliver Stolpe amesema, “njia ya Afghanistan kupambana na kilimo haramu inahitaji uwekezaji wa muda mrefu na wa pamoja kupitia ushirikiano wa kimataifa. Ni muhimu kuwawezesha wakulima kupata vyanzo mbadala vya kipato, kuimarisha juhudi za kutokomeza mimea haramu na kudhibiti biashara ya madawa ya kulevya”.
Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na Kaimu Mkuu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi Nchini Afghanistan UNAMA, Roza Otunbayeva amesema; “tatizo la madawa ya kulevya la Afghanistan si la ndani pekee. Linahusisha wahusika wa ndani na wa kimataifa, hivyo linahitaji ushirikiano mpana katika kudhibiti usambazaji, mahitaji na biashara ya madawa hayo”…/