Dar es Salaam. The music’s for the sad man. Ni moja ya mistari iliyopo katika wimbo wa rapa kutokea Marekani, Jay Z, Young Forever (2009), kwa tafsiri isiyo rasmi akimaanisha – Huu muziki ni kwa ajili ya mtu mwenye huzuni!.

Mr. Hudson ambaye ameshirikishwa katika ngoma hiyo, ndiye ameimba sehemu hiyo ambayo imepata umaarufu zaidi mtandaoni baada ya mke wa Jay Z, Beyonce Knowles kuirudia katika ziara yao, On The Run 2014.

Hata hivyo, gwiji wa muziki wa Soukous nchini marehemu Remmy Ongala kupitia wimbo wake, Muziki Asili Yake Wapi (1989), anasema muziki hauna mwenyewe, bali muziki ni mwito, fundisho, maombolezo na kilio.

Remmy aliyefariki Desemba 2010 akiwa na umri wa miaka 63, anaenda mbali zaidi na kusema hata yeye usimuone akiimba ukadhani anayo furaha, kumbe anayo huzuni moyoni mwake.  

“Ukiwa na sherehe utaimba nyimbo za furaha, ukiwa na tabu utaimba nyimbo za masikitiko,” anaimba Remmy katika wimbo huo na kuongeza.

“Ukifa leo utapelekwa kaburini na nyimbo za maombolezo. Ni muziki pekee ulio na nguvu, utawakusanya wabaya na wazuri siku ya mwisho Mungu akitoa hukumu,” anaeleza Remmy Ongala.

Mkali wa Rock na Blues, Elton John aliwahi kusema kuwa muziki una nguvu ya uponyaji amini usiamini, ndio tiba pekee duniani inayoweza kukutoa kutoka kwenye lindi la mawazo na maumivu angalau kwa saa chache.

Kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2015 na Chuo Kikuu cha Loma Linda cha California, ulibaini kwamba wagonjwa 100 waliowekwa katika chumba chenye muziki bila kupewa dawa walipona haraka kuliko waliopewa dawa!

Utafiti huo wa wanafunzi wa kitengo cha afya (School of Behavioral Health), ulieleza kuwa muziki ni jambo la ulimwengu wote ambalo lina athari za kiutambuzi, kimhemko na kisaikolojia kwa wanadamu.

Na miongoni mwa athari hizo ni za kimatibabu kama vile kupunguzwa kwa dalili za kupata magonjwa ya mwili na akili. Huo ndio muziki.

Aliyekuwa Rais wa Iraq, Saddam Hussein kuelekea muda wake wa mwisho (Super Twelve) ambao alikuwa anasubiria kunyongwa, inadaiwa alipenda sana kusikiliza nyimbo za Mary J. Blige, Malkia wa Hip Hop Soul na RnB.

Hiyo ni kwa mujibu wa Will Bardenwerper ambaye alikuwa miongoni mwa Wanajeshi 12 wa Marekani waliokuwa wanamlinda Saddam wakati akisubiria kunyongwa mwaka 2006.

Ameeleza hayo kupitia kitabu, The Prisoner in His Palace, His American Guards, and What History Left Unsaid (2017) – Mfungwa ndani ya kasri lake, walinzi wake wa Kimarekani na kile ambacho historia ilikiacha bila kukisema.

Ndipo linatimia neno la Mr. Hudson – Huu muziki ni kwa ajili ya mtu mwenye huzuni. Na kabla ya kusema hayo, Mr. Hudson alitanguliza ujumbe mwingine mzito unaotupa picha kwanini alifikia hatua ya kusema hivyo.

“Let us die young or let us live forever. We don’t have the power, but we never say never… Life is a short trip(Acha tufe tukiwa vijana au tuishi milele. Hatuna nguvu hiyo, lakini hatukati tamaa… Maisha ni safari fupi)” anaimba Mr. Hudson.

Mstari huo unafana kiasi na ule wa Whitney Houston katika wimbo wake, My Love is Your Love (1999) uliobeba jina la albamu yake ya nne, huku pia ukishika nafasi ya nne katika chati ya Billboard Hot 100.

“If I should die this very day, Don’t cry, ‘cause on Earth, we wasn’t meant to stay (Kama nitakufa leo hii, usilie, kwa sababu duniani hatukuumbwa tuwe wa kudumu)” anaeleza Whitney Houston.  

Whitney, mkali wa Soul, RnB na Pop aliyefariki akiwa na umri wa miaka 48 hapo Februari 2012, alitumia miaka 27 ya maisha yake akiimba muziki ulioburudisha na kuponya nyoyo za wengi hasa wenye huzuni.

Kama alivyosema Remmy Ongala kuwa muziki ni maombolezo, nyimbo za namna hiyo zimekuwa zikirejea kwenye chati mara kwa mara na hata kupata wasikilizaji wengi maana zimekuwa sehemu ya maisha ya watu wengi.

Mmoja wapo ni ule wa rapa Wiz Khalifa, See You Again – Tutaona Tena (2015), ambao video yake inashika nafasi ya pili duniani kwa kutazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube, na nafasi ya kwanza upande wa Hip Hop.

Ukiwa umetazamwa zaidi ya mara bilioni 6.8 YouTube, wimbo huu unaelezea huzuni ya kumpoteza mtu muhimu maishani, lakini pia unaonyesha tumaini la kuonana tena huko mbinguni au peponi.

Mistari yake inasisitiza urafiki wa kweli, upendo, na kumbukumbu nzuri zinazobaki hata baada ya kifo. Unatoa ujumbe wa faraja na matumaini, kwamba ingawa maisha yana mwisho, uhusiano wa kweli huishi milele.

Akimshirikisha Charlie Puth, Wiz Khalifa alitoa wimbo huo kwa ajili ya kumuenzi marehemu Paul Walker, aliyekuwa mwigizaji wa filamu maarufu ya Fast & Furious, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mwaka 2013.

Na mwaka 2015, ‘See You Again’ ulikuwa ndio wimbo uliouzwa zaidi duniani, na sasa Chama cha Rekodi za Muziki Marekani (RIAA) kinautaja kufikia mauzo ya Diamond, yaani umeuzwa au kusikilizwa kwa kiwango kinacholingana na nakala milioni 10.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *