Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Malaysia imetangaza kwamba takriban watu 290 bado hawajulikani walipo leo Jumapili baada ya boti iliyokuwa imebeba watu wapatao 300 kuzama karibu na mpaka wa Malaysia na Thailand, huku manusura 10 wakiokolewa na mwili mmoja kupatikana.

Admirali Romley Mustafa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Baharini katika majimbo ya Kedah na Perlis kaskazini mwa Malaysia, amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba kuna wahanga wengine waliofariki dunia katika ajali hiyo ambao bado wko baharini, yapata siku tatu baada ya mashua hiyo kuzama. Boti hiyo ilikuwa ikitokea Buthidaung huko magharibi mwa Myanmar.

Shirika la habari la kitaifa la Malaysia, Bernama, limemnukuu mkuu wa polisi wa Kedah, Adli Abu Shah akisema, “Wahamiaji hao waliokuwa wakielekea Malaysia awali walipanda meli kubwa, lakini walipokaribia mpaka waliagizwa kuhamia kwenye boti tatu ndogo ili kuepuka kuonekana na mamlaka husika.”

Waislamu wa jamii ya Rohingya walio wachache nchini Myanmar wamekuwa wakikimbia nchi yao kutokana na ukatili na mauaji yanayofanywa na  Mabudha waliowengi. Jamii ya Waislamu hao imenyimwa haki zote za uraia na hukabiliwa na unyanyasaji wa kutisha.

Abu Shah amesema kwamba hatima ya boti zingine mbili bado haijajulikana na kwamba operesheni ya utafutaji na uokoaji bado inaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *