
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vilikusanya mamia ya miili kutoka mitaani na vitongoji vya makazi ya raia vya El Fasher (mji mkuu wa Darfur Kaskazini) na kuzika baadhi ya miili hiyo katika makaburi ya umati, huku mingine ikichomwa moto kabisa.
Mtandao huo umeongeza katika taarifa yake ya leo Jumapili kwamba RSF imefanya mojawapo ya “matendo ya kinyama zaidi” katika mji wa El Fasher katika siku za hivi karibuni.
Taarifa hiyo imeelezea kilichotokea kuwa ni “ukurasa mpya wa mauaji ya kimbari.”
Mtandao huo umesisitiza kwamba vitendo hivyo vinawakilisha ukiukwaji mkubwa wa kanuni zote za kimataifa na kidini zinazowahakikishia wahanga haki ya kuzikwa kwa heshima na kuzuia kukatwa viungo vya miili ya maiti.
Taarifa hiyo pia imeubebesha Uongozi wa RSF dhima kamili ya “uhalifu” huo, na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua “hatua za haraka za kuanzisha uchunguzi huru wa kimataifa” kuhusu uhalifu unaoendelea kufanywa katika mji wa El Fasher.
Madaktari wa Sudan wameongeza kuwa kinachoshuhudiwa huko Darfur “kimevuka mipaka ya janga la binadamu na kuwa mauaji ya kimbari ya kimfumo yanayolenga maisha na utu wa binadamu, huku kukiwa na ukimya wa kimataifa unaofanana na ushiriki katika uhalifu unaofanyika.”
Madai haya yanakuja wiki kadhaa baada ya Vikosi vya Msaada wa Haraka kudhibiti mji wa El Fasher mwishoni mwa Oktoba, na kuua mamia ya watu huku maelfu ya raia wakikimbia makazi yao.
Awali, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan ilithibitisha kwamba mji wa El Fasher umeshuhudia “ongezeko la mashambulizi ya kikatili” katika siku kumi zilizopita, ikieleza kuwa mamia ya raia, wakiwemo wanawake na watoto wameuawa, na maelfu ya wengine, wakiwemo wafanyakazi wa matibabu na waandishi wa habari wamechukuliwa mateka.