Matokeo ya majanga ya mabadiliko ya tabianchi tayari yameshawalazimisha mamilioni ya watu ulimwenguni kuwa wakimbizi, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) iliyotolewa siku ya Jumatatu (Novemba 10) wakati ulimwengu ukianza mkutano wa 30 wa kilele unaofanyika nchini Brazil.
“Kwa muongo mmoja uliopita, majanga yanayohusiana na hali ya hewa yamesababisha wakimbizi wa ndani milioni 250 ulimwenguni, sawa na wakimbizi 67,000 kwa siku.” Ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Shirika hilo ilizungumzia juu ya kile ilichokiita “mduara wa papo kwa papo wa migogorona majanga ya mabadiliko ya tabianchi”, ambapo robo tatu ya wakimbizi hao wanaishi kwenye maeneo yaliyo hatarini zaidi kuathirika kwa majanga ya kimazingira.
UNHCR iliyataja mafuriko nchini Sudan Kusini na Brazil, kiwango kikubwa cha joto nchini Kenya na Pakistan, na ukosefu mkubwa wa maji nchini Chad na Ethiopia kama mifano ya majanga hayo.
Ripoti hiyo ilibainisha kwamba mabadiliko ya tabianchi “yanaongeza na yanaimarisha changamoto zinazowakabili wale ambao tayari wameshakuwa wakimbizi, na pia wenyeji wao, hasa kwenye mazingira tete na yenye migogoro mingine.”
Uhaba wa fedha kuhudumia wakimbizi
Hata hivyo, kwa mujibu wa UNHCR, ni robo tu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuyasaidia mataifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ndiyo iliyofika kwa nchi hizo, ambazo ndizo zinazowahifadhi wakimbizi wengi zaidi.
Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi, COP30, kawaida hutumika kama jukwaa la mataifa masikini kutoa wito wa fedha kwa mataifa yaliyoendelea ili kukabiliana na hali mbaya ya hewa inayosababishwa na mataifa tajiri.
“Ikiwa tunataka utulivu, lazima tuwekeze kule ambako watu wako hatarini. Kuzuwia wakimbizi zaidi, ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi unahitaji kuzifikia jamii ambazo tayari zipo kwenye ukingo wa kutumbukia shimoni.” Alisema mkuu wa shirika la UNHCR, Fillipo Grandi.
Shirika hilo lilisema kuwa kufikia katikati ya mwaka wa 2025, watu milioni 117 walikuwa tayari wameshageuzwa wakimbizi kutokana na vita, migogoro na mauaji. Idadi ya nchi zinazokabiliwa na hali mbaya ya hewa inatazamiwa kutoka tatu hadi 65 ifikiapo mwaka 2040, ambazo ndizo zenye zaidi ya asilimia 45 ya wakimbizi wote ulimwenguni.
Hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kukata msaada wa nchi yake kwenye miradi ya UNHCR inatajwa kuathiri pakubwa hali za wakimbizi walio kwenye mataifa yanayokabiliwa na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi.
Marekani ilikuwa ndiye mfadhili mkubwa wa shirika hilo, ikichangia asilimia 40 ya fedha zake.