Dar es Salaam. Rapa kutoka kundi la Weusi, G Nako ameendelea kuwa mfano wa msanii anayekua na kubadilika kulingana na mabadiliko ya soko la muziki, kitu kinachofanya jina lake kuzidi kuwepo katika tasnia miaka nenda rudi.
G Nako, mwanachama wa zamani wa Nako 2 Nako Soldiers anasifika kwa mtindo wake wa kuchanganya rap na uimbaji, hivyo kuwa nguzo muhimu katika makundi yake yote ya muziki. Fahamu zaidi.
1. Mara zote anapoenda studio kurekodi, kati ya vitu ambavyo G Nako anahakikisha anakuwa navyo, basi ni chupa ya chai ili kuweka sawa koo lake kwa ajili ya kutengeneza muziki mzuri.
2. Mke wa G Nako, Yasinta ndiye aliyetokea kwenye video ya wimbo wa rapa huyo, Mama Yeyoo (2013), wakati video ya wimbo huo aliyomshirikisha Ben Pol inaachiwa, wawili hao walikuwa bado hawajaoana.
3. G Nako ambaye alifunga ndoa na Yasinta hapo Desemba 2019, mkewe huyo ndiye mara nyingi humshauri ni wimbo upi wa kutoa, na ndiye huwa mtu wa kwanza kumzikilisha wimbo baada ya kurekodi.
4. Mbali na muziki, G Nako ni msanii mwenye mtazamo wa kibiashara na ubunifu mkubwa, akijihusisha pia na tasnia ya mitindo hasa upande wa mavazi, biashara ambayo anafanya kwa kushirikiana na mkewe.
5. Nyimbo 10 za G Nako zinazoongoza kwa kutazamwa YouTube, zote amefanya kolabo na wasanii wengine ambapo mbili za mwanzo ni zile alizoshirikiana na Diamond Platnumz (Komando) na Zuchu (Hapo).
6. Wakati Weusi wanashuti video ya wimbo wao, Wapoloo (2019), G Nako hakuwepo hivyo baadhi ya vipande vyake katika video hiyo alishuti peke yake kisha akatuma kwa director wa video hiyo, kazi ikamalizika hivyo.
7. Ni G Nako na Joh Makini pekee ambao hawajawahi kukosekana katika wimbo wowote wa Weusi tangu kundi hilo lilipoibuka na wimbo wake, Gere (2013) ulioshinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA) 2014.
8. Bonta alikosekana katika albamu yao, Air Weusi (2021), Lord Eyes katika wimbo, Mdundiko (2018), huku Nikki wa Pili kwenye nyimbo kama Waoshe (2021), Hujabalehe (2022), Booty Hammer (2024) na kadhalika. Ikumbukwe Weusi wamefanikiwa kutoa wimbo mmoja tu ambao umekutanisha wasanii wote watano wa kundi hilo. Wimbo huo, Watoto wa Mungu (2013), ulitoka chini ya Bongo Records kwa P-Funk Majani.
9. G Nako na Lord Eyes walitokea kundi la Nako 2 Nako kisha wakajiunga na Nikki wa Pili, Joh Makini na Bonta ambao nao walitokea kundi la River Camp, kisha watano hao wakanzisha kundi la Weusi.
10. Hata hivyo, awali Lord Eyes alikuwa na kundi la Hood Squard Hardcore Unit, akiwa na wenzake, JCB na Spark Dogg, baadaye akaungana na G Nako na Bou Nako kutokea Chronic Mob ndipo wakaunda Nako 2 Nako.