
Dar es Salaam. Katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kijamii, kisiasa na kiuchumi, elimu ya amani inazidi kuthibitisha umuhimu wake kama nguzo kuu ya kulinda utulivu wa taifa.
Watanzania tunahitaji kufahamu kuwa amani si tu ukosefu wa vita, bali ni hali ya utulivu wa ndani unaojengwa kupitia elimu, uelewa, na nidhamu ya kimaadili katika jamii.
Ni matokeo ya juhudi za pamoja za watu wanaotambua wajibu wao kwa taifa, familia na vizazi vijavyo.
Kwa muda mrefu, nimekuwa nikitazama kwa makini mwenendo wa vijana katika mijadala ya kijamii na hata mitandaoni, na kubaini kuwa wengi wanahitaji maarifa zaidi kuhusu namna bora ya kudai haki zao bila kuvunja misingi ya kisheria. Mara nyingi ushawishi wa watu wachache wenye maslahi binafsi, umekuwa ukisababisha uamuzi usio sahihi ambao baadaye huleta madhara kwa jamii nzima.
Hapa ndipo elimu ya amani inapokuwa dira inayotupa uwezo wa kutofautisha kati ya hoja ya kujenga na ile ya kubomoa.
Amani ni matokeo ya fikra chanya, za mtu mmoja mmoja na za jamii kwa ujumla. Pale ambapo fikra zinajengwa katika msingi wa elimu, uelewa na upendo wa kweli kwa nchi, ni vigumu kuona migogoro inayoibuka kwa urahisi.
Elimu ya amani na saikolojia inasaidia mtu kutafakari matokeo ya vitendo vyake, kujifunza kuheshimu maoni ya wengine na kujenga subira katika majadiliano. Ndiyo maana jamii zenye watu walioelimika kimaadili huweza kuhimili tofauti za kisiasa, kidini au kiitikadi bila kuingia katika mifarakano.
Kwa mtazamo wangu, elimu ya saikolojia ya jamii inapaswa kupewa uzito mkubwa shuleni na vyuoni. Hii itawasaidia vijana kuelewa hisia zao, kudhibiti mihemko na kutathmini ushauri wanaopewa na baadhi ya watu kabla ya kuchukua hatua.
Uelewa huu wa kisaikolojia ni silaha ya kiakili inayomkinga kijana dhidi ya ushawishi hasi unaoweza kumwongoza kwenye mienendo mibaya kama matumizi ya vilevi, biashara haramu za mwili, mihadarati au uhalifu wa aina yoyote. Vijana wakielewa thamani ya utulivu wa akili, wataweza kufikiri kwa kina kabla ya kushawishika kuingia katika makundi au matendo yanayohatarisha amani.
Aidha, ni muhimu kutambua kuwa saikolojia ya jamii haiishii katika madarasa pekee, bali inapaswa kuanza majumbani. Wazazi na walezi wanapaswa kuwa walimu wa kwanza wa amani. Lugha wanazotumia, jinsi wanavyoshughulikia migogoro ya kifamilia na namna wanavyowalea watoto katika kuheshimu tofauti, vyote vina mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa misingi ya utulivu wa jamii.
Wataalamu wa afya ya akili wanasisitiza kuwa uamuzi sahihi hutokana na akili iliyo tulivu na yenye afya. Vijana wanapojifunza kudhibiti msongo wa mawazo, wanakuwa na uwezo wa kupanga maisha yao kwa umakini na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ufanisi.
Hata mafundisho ya dini zetu yanasisitiza umuhimu wa kudhibiti nafsi, kujiepusha na maovu, na kufanya mema kwa jamii, misingi ambayo yote ni sehemu ya elimu ya amani.
Dini zote zinahimiza upendo, uvumilivu, na heshima, misingi inayofanya jamii iwe imara na yenye mshikamano.
Ni rai yangu kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuingiza somo la elimu ya amani na saikolojia ya kuhimili misongo ya maisha katika mitalaa ya elimu. Vijana wengi wanapohitimu masomo wanakumbana na changamoto za kiuchumi, kukosa ajira au kutokuelewa mwelekeo wa maisha yao.
Bila maandalizi ya kisaikolojia, wengi hukata tamaa au kuchukua uamuzi usio sahihi kama kujihusisha na uhalifu, utumiaji wa dawa za kulevya au hata kujiua. Kuwaandaa vijana kisaikolojia ni kuwapa silaha ya kukabiliana na maisha halisi bila kupoteza matumaini.
Vilevile, taasisi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari na viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana katika kueneza elimu ya amani. Vyombo vya habari vinaweza kutumia nafasi zao kufundisha umma juu ya uvumilivu, nidhamu na kuheshimu misimamo tofauti badala ya kusambaza maneno ya kuchochea migawanyiko. Amani haijengwi kwa maneno matupu, bali kwa matendo, kwa uamuzi wa kila mmoja wetu kutanguliza busara kabla ya hasira.
Amani inajengwa, inalindwa na kuendelezwa kwa maarifa, si kwa bahati. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuwa balozi wa amani, kuielimisha jamii, na kulinda utulivu huu uliojengwa kwa gharama kubwa. Bila amani, maendeleo hayana msingi, lakini kwa elimu ya amani, hata changamoto ngumu zinaweza kutatulika.
Fatma Jalala ni mwandishi wa habari. 0655847002