Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Wapalestina, Hamas, imelaani vikali hatua ya Bunge la Israel (Knesset) kupitisha kwa mara ya kwanza mswada unaoruhusu kunyongwa kwa Wapalestina waliotekwa, ikikitaja kama mwendelezo wa sera za kibaguzi na jinai za utawala wa Kizayuni.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, Hamas ilisema: “Kupitishwa kwa mswada huu na kile kinachoitwa Knesset ya Kizayuni ni mwendelezo wa sera za kibaguzi na jinai za utawala wa Kizayuni, na ni jaribio la kuhalalisha mauaji ya halaiki dhidi ya watu wetu wa Palestina wanaoishi katika hali ya kukaliwa kwa mabavu ardhi yao .”

Jumatatu, wabunge wa utawala huo waliidhinisha mswada huo kwa kura 39 dhidi ya 16, hatua inayoupeleka kwa Kamati ya Usalama wa Kitaifa ya Knesset kwa mazungumzo na upigaji kura wa mwisho kabla ya kuwa sheria.

Wiki iliyopita, Kamati hiyo ya Usalama wa Kitaifa iliidhinisha mswada huo na kuufikisha kwa Bunge Kuu la Knesset kwa mjadala na uamuzi wa mwisho.

Hamas ilieleza kuwa mswada huo ni wa “kifashisti na kikatili,” ikikemea Israel kwa kukiuka waziwazi sheria na mikataba ya kimataifa, ikiwemo Sheria ya Kibinadamu ya Kimataifa na misingi ya haki za binadamu.

Taarifa ya Hamas imetoa wito kwa jumuiya za kimataifa, Umoja wa Mataifa, na mashirika yote ya haki za binadamu kulaani ‘sheria’ hii hatari ya kibaguzi na kukishinikiza ifutwe.

Harakati hiyo pia ilitaka kuundwa kwa kamati za uchunguzi za kimataifa kutembelea magereza ya Israeli na kuchunguza hali ya Wapalestina waliotekwa, ikisema wanakabiliwa na “mateso ya kimfumo na unyanyasaji” ambao umepelekea vifo vya makumi yao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina wiki iliyopita ilitaja mswada huo kuwa ni jinai ya kivita na ishara ya kuongezeka kwa misimamo mikali na uhalifu wa utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *