Mbinu hii yenye vipengele vingi iliwaunganisha wadau mbalimbali, wakiwemo wanajamii, taasisi za serikali kama Mamlaka ya Jiji la Kampala (KCCA) na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), pamoja na washirika kutoka sekta binafsi, ili kubuni na kutekeleza suluhisho thabiti na endelevu. Pricila Asiku, Meneja wa Mradi kutoka kampuni ya Adroit Consult International, anafafanua hali halisi ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko na jinsi mradi huu wa UNDP unavyolenga kuyasaidia.

Anaema “Baadhi ya mitaa kama Chigundo na Sina katika Makerere Kavule yameathirika zaidi na mafuriko kutokana na ukosefu wa mifereji, ujenzi holela, taka nyingi na mvua kubwa zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi. Kupitia kituo cha UNDP, tulianzisha jaribio la maarifa ya pamoja katika maeneo ya Chigundo na Sina, tukichunguza kama jamii na taasisi zinaweza kushirikiana kubuni na kujenga mifereji midogo kwa gharama nafuu ili kupunguza hatari ya mafuriko katika maeneo haya hatarishi, jaribio ambalo lililenga kujibu maswali muhimu katika maeneo makuu manane ya utafiti.”

Wakazi wa Makerere Kavule wamekuwa mashahidi wa mabadiliko yanayoletwa na mradi huu. Zziwan N. Charles, mmoja wa wawakilishi wa jamii, anakumbuka hali ilivyokuwa kabla ya mradi kuanza.

Anasema, “Maji yalikuwa yakienea kila mahali katika nyumba hizi, na watu walilazimika kuyachota kwa mikono. Maji yalikuwa yanatoka juu kwa wingi, hayakuwa na njia ya kupita. Watu wetu, huelekeza taka zao kokote kule, jambo linalozidisha tatizo. Mwishoni mwa mwaka jana tulialikwa Entebbe kwa ajili ya uzinduzi wa mradi huu, na baada ya hapo jukumu likakabidhiwa rasmi kwa UNDP ili utekelezaji uanze.”

Kwa wakazi wa eneo hilo, mabadiliko ni dhahiri. mkazi wa Kiggundu ambaye jina lake limehifadhiwa anaeleza tofauti kubwa kati ya hali ya sasa na zamani kabla ya mfumo mpya wa mifereji kuanzishwa.

Mmoja wao anasema “Wakati wa mvua, mafuriko yalikuwa makubwa sana na yalileta uharibifu mwingi. Maji yalikuwa mengi kiasi kwamba mtu mzima angepata shida kutembea. Ukitaka kumpeleka au kumchukua mtoto shule, ilibidi umbebe kichwani kuvuka maji. Lakini sasa kuna mabadiliko. Mvua inaponyesha, maji hayatuami kama zamani. Yanapita haraka zaidi, na eneo halifuriki tena kama hapo awali.”

Kupitia maarifa ya pamoja, wakazi wa Makerere Kavule sasa wanaishi katika mazingira salama zaidi, huku uzoefu wao ukiwa mfano wa kuigwa kwa miji mingine inayokabiliwa na changamoto kama hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *