
Muda unaisha haraka kuweza kuzuia baa la njaa katika maeneo yenye kutia wasiwasi zaidi, inaeleza taarifa ya pamoja ya FAO na WFP iliyotolewa leo jijini Roma Italia yaliko makao makuu ya mashirika haya mawili ya Umoja wa Mataifa. Taarifa inafafanua kwamba migogoro, miyumbo ya kiuchumi, hali mbaya ya hewa, na upungufu mkubwa wa fedha vinaendelea kuzidisha hali hii. Licha ya kuongezeka kwa uhitaji wa kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa kiwango kikubwa, ufadhili ni mdogo kwa kiwango cha kutisha.
Ripoti hiyo mpya wanayoizungumzia kuhusu maeneo yanye njaa duniani ikiwa inaangazia kuanzia kipindi cha mwezi huu wa Novemba hadi mwezi Mei mwaka kesho 2026, inaonesha kuwa katika maeneo 14 kati ya 16 yaliyotambuliwa, migogoro na vurugu ndizo sababu kuu za njaa.
Ripoti inabainisha nchi na maeneo sita yenye wasiwasi mkubwa zaidi kuwa ni Haiti, Mali, Palestina, Sudan Kusini, Sudan na Yemen ambako watu wanakabiliwa na hatari ya karibu ya njaa ya kiwango cha maafa yaani ngazi ya 5 ya vipimo vya uhakika wa chakula.
Nchi nyingine sita zimeainishwa kuwa katika viwango vya upatikanaji wa chakula vya mashaka makubwa nazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Myanmar, Nigeria, Somalia, na Syria
Maeneo manne mengine ni Burkina Faso, Chad, Kenya, na hali ya wakimbizi wa Rohingya walioko nchini Bangladesh.
Kadri maeneo haya yenye njaa yanavyozidi kukaribia hali ya maafa au baa la njaa, ufadhili wa kibinadamu unazidi kuwa mdogo kwa kiwango cha hatari. Kufikia mwisho wa mwezi ulipita yaani Oktoba 2025, ni dola bilioni 10.5 pekee kati ya dola bilioni 29 zinazohitajika kwa watu walio katika hatari kubwa ndizo zilikuwa zimepatikana.
Upungufu huu mkubwa wa fedha unalemaza juhudi za dharura, unasababisha kupunguzwa kwa mgao wa chakula, na kupunguza upatikanaji wa chakula kwa makundi yaliyo hatarini zaidi, huku msaada wa chakula kwa wakimbizi ukifikia kiwango cha kuvunjika.
Utoaji wa msaada umepungua katika maeneo mengi yenye njaa. WFP imelazimika kubana vigezo vya kutoa msaada na kupunguza msaada kwa wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makazi yao. Wakati huo huo, programu muhimu za lishe na chakula shuleni zimesitishwa katika baadhi ya nchi, na kuwaacha watoto, wakimbizi, na familia zilizo hama makazi zikiwa katika hatari kubwa.
FAO inaonya kuwa ukosefu wa fedha pia unadhoofisha juhudi za kulinda kilimo, ambacho ni muhimu kwa ustawi wa uzalishaji wa chakula na kuzuia majanga ya mara kwa mara. Bila fedha za haraka, msaada muhimu wa kilimo kama mbegu, huduma za afya ya mifugo, na hatua za mapema za kilimo hautafikia jamii kabla ya misimu ya upandaji au kabla ya majanga mapya kutokea. Hii itapunguza uwezo wa jamii kujitegemea na kuongeza hatari ya migogoro mipya ya chakula.
Katika nchi zote zilizo kwenye orodha ya maeneo hatarishi ya njaa, uzalishaji wa chakula wa kaya na kipato havitoshelezi mahitaji ya msingi. Programu zinazojenga uwezo wa kustahimili misukosuko sasa ni muhimu ili kulinda riziki na kupunguza utegemezi wa misaada ya dharura.
Kuzuia njaa kabla haijachelewa
FAO na WFP zinasisitiza kwamba njaa inaweza kutabirika na pia inaweza kuzuilika. Kwa pamoja, mashirika haya yanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuelekeza upya umakini katika kuzuia njaa na kuongeza uwekezaji katika uhakika wa chakula wa muda mrefu na uhimilivu.
FAO na WFP zinatoa wito kwa serikali, wafadhili, na washirika kuchukua hatua za haraka kulingana kabla hali haijafikia kiwango cha maafa. Hatua za mapema yaani msaada kabla ya janga kutokea huwezesha jamii kustahimili mishtuko ya njaa, na ni nafuu zaidi kuliko kutoa misaada baada ya hali kuwa mbaya. Wakati huo huo, uwekezaji endelevu katika ujenzi wa uhimilivu ni muhimu ili kulinda riziki za vijijini na kuzuia kuongezeka kwa njaa.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu anasema, “mifumo ya tahadhari ya mapema duniani inafanya kazi jambo hili ni la msingi kwa kuchukua hatua mapema, tunapaswa kutoka katika hatua ya kukabiliana na majanga baada ya kutokea hadi kuzuia kabla ya kutokea. Kuwekeza katika maisha ya watu, mnepo na ulinzi wa kijamii kabla njaa haijafikia kiwango cha juu kutaokoa maisha na rasilimali. Kuzuia njaa si wajibu wa kimaadili pekee ni uwekezaji wenye busara katika amani na uthabiti wa muda mrefu. Amani ni sharti la usalama wa chakula, na haki ya kupata chakula ni haki ya msingi ya binadamu.”
WFP na FAO pia wanasisitiza haja ya ufikiaji wa misaada ya kibinadamu bila vizuizi katika maeneo yenye migogoro, ili chakula, lishe, na misaada ya kilimo ipatikane kwa wale wanaohitaji zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain anasema, “tuko kwenye ukingo wa janga la njaa ambalo linaweza kuzuilika kabisa, na linatishia kusababisha vifo vya watu wengi katika nchi kadhaa, akina mama wanakosa kula ili watoto wao wapate chakula, na familia zinamaliza kile kidogo walichonacho wakijaribu kuendelea kuishi. Tunahitaji fedha mpya na upatikanaji usio na vizuizi kushindwa kuchukua hatua sasa kutachochea zaidi hali ya kutokuwepo kwa utulivu, uhamaji wa watu, na migogoro.”
FAO na WFP zinasisitiza kwamba njaa inaweza kuzuilika, lakini ni lazima kuwe na nia ya kisiasa, uongozi, ufadhili wa kutosha, na uwajibikaji wa pamoja. Maisha ya mamilioni ya watu yanategemea hatua za haraka sasa.
Ripoti ya Hunger Hotspots hutolewa mara mbili kwa mwaka kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia Global Network Against Food Crises (GNAFC).