
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema, nchi yake haitakubali mahubiri yanayotolewa na Umoja wa Ulya EU kuhusu jinsi inavyoendesha shughuli zake za usalama wa taifa na akapuuza ukosoaji wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Marekani kuzilenga boti zinazopita eneo la Carribean.
Vikosi vya jeshi la Marekani vimeshashambulia vyombo vya baharini visivyopungua 20 katika pwani ya Venezuela, vikidai kuwa vimehusika katika “ugaidi wa madawa ya kulevya.” Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na nchi za Ulaya wanachama wa shirika la kijeshi la NATO, zimehoji kama mashambulizi hayo yana uhalali kulingana na sheria za kimataifa.
“Sidhani kama Umoja wa Ulaya una uwezo wa kuainisha sheria za kimataifa ni nini, na kile ambacho kwa hakika haziwezi zaidi kuwa na uwezo wa kuainisha ni vipi Marekani ilinde usalama wake wa taifa,” Rubio ametamka hayo mbele ya waandishi wa habari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameendelea kueleza kuhusu serikali hizo hizo za Ulaya zinazokosoa vitendo vya Washington akisema zenyewe: “zinataka tutume na kusambaza, kwa mfano, makombora ya Tomahawk yenye uwezo wa nyuklia ili kutetea Ulaya, lakini Marekani inapoweka manowari za kubeba ndege za kivita katika eneo letu tunakoishi, kwa namna fulani hilo huwa ni tatizo.”
Russia pia imelaani mashambulizi ya jeshi la Marekani katika eneo la Carribean ikisema kuwayanafanywa kinyume cha sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov alibainisha wiki hii kwamba hatua za Washington za kupambana na uhalifu wa madawa ya kulevya ingepasa zichukuliwe kwa ufanisi zaidi nchini Ubelgiji, ambayo jaji mmoja wa nchi hiyo hivi karibuni aliielezea Ubelgiji kuwa inabadilika na kuwa “nchi ya madawa ya kulevya”…/