Dar es Salaam. Waswahili wanasema cha kale dhahabu, lakini dhahabu isipong’arishwa haiwezi kuwa na thamani machoni mwa watu. Ndivyo pia ilivyo katika maisha ya sanaa hasa kwa wasanii wakongwe, ili wawezi kupanda chati kama mwanzo ni lazima ubunifu uongezeke kulingana na wakati uliopo.

Mwananchi imetupia jicho kwa mchekeshaji mkongwe Rashid Mwinshehe maarufu kama Kingwendu, amefunguka namna ambavyo wasanii wa zamani wa vichekesho wanavyoshindwa kurudi kwenye gemu kutokana na kushindwa kuandika stori.

“Wasanii wa zamani wengi wetu tumekuwa hatuna vitu vipya. Hiyo ndiyo changamoto yetu kubwa katika tasnia hii na hatuwezi kuandika stori kwa mtindo huu wa kisasa kulingana na wakati uliopo, lakini kama tukielekezwa namna ya kuendana na soko naimani tutakuwa vizuri,” amesema.

Akizungumzia ujio wa wachekeshaji wapya Kingwendu amepongeza hasa katika uchekeshaji wima ‘Stand Up Comedy’ kwa kusema imekuwa chachu ya tasnia ya vichekesho kukua kwa kasi nchini kila kukicha.

“Ujio wa wachekeshaji chipukizi unaendeleza sanaa hasa kwa wachekeshaji wa majukwaani. Ila tunawaomba wakumbuke kufanya kazi na wazee, yapo mambo wanaweza wakajifunza kutoka kwetu. Wakati mwingine hata watunzi wa filamu, wajue tunaweza kuigiza scene ambazo siyo za kuchekesha tu,” amesema Kingwendu.

Aidha ameeleza kuwa kuna wakati wachekeshaji wakongwe wanaweza kupewa nafasi lakini siyo ambazo zitawaonesha au kurudisha majina yao huku akitolea mfano baadhi ya nafasi kama vile uhusika wa kuigiza ulinzi wa getini.

“Kuna wakati mwingine hata wakitupa nafasi wanaona tunafaa kukaa kama walinzi kukatakata viuno, kuna wakati ninaweza nikaigiza kama mjomba, baba ama babu,” amesema.

Utakumbuka wapo baadhi ya waigizaji wakongwe bado wanatikisa kwenye gemu kama vile Muhogo Mchungu anayeigiza kwenye tamthilia ya Huba, Bi Staa yupo kwenye Jua Kali na wengine wengi.

Licha ya hayo mwigizaji huyo anasema nje na sanaa anafanya shughuli ya kilimo cha biashara, Wilaya Kisarawe katika kijiji cha Malumbo.

“Kupitia kilimo nimeona vijana wengi katika wilaya hiyo, wamefungua maduka, wamenunua bodaboda, maisha yao yamebadilika, nimekuwa nikiwashauri watu wengi kuwekeza katika kilimo.

“Panapo uzima, nawaza kulima matikiti, kwani shamba langu linakubali zao hilo, nione litaniingizia faida kiasi gani kwa sasa nalima mihogo,” amesema

Wakati akisema hayo hakuacha kukumbusha enzi zake kabla ya sanaa ambapo alikuwa akifanya kazi ya udalali wa nyumba na viwanja na ndipo huko akakutana na mkewe.

“Kabla ya kuanza sanaa mwaka 2000, nilikuwa dalali wa nyumba za kupanga na kuuza viwanja. Nakumbuka nikiwa kwenye harakati hizo nilikutana na mkewe  wangu ambaye naishi naye hadi sasa.

“Udalali wa zamani tulikuwa smati, ukitoka kwenda kijiweni kupanga mipango ya kazi, unapiga suti, tai, kiatu kimepigwa dawa, pia hatukuwa matapeli, kwani tulitambua sheria,” amesema.

Ubunge ulivyomfilisi

Utakumbuka mwaka 2015 aligomba ubunge wa Jimbo la Kisarawe, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), anasema katika harakati hizo  alipoteza  takribani Sh 28 milioni katika kampeni.

“Nilitumia takribani Sh28 milioni katika kampeni zangu, kulipa wasanii, magari ya kubeba wanachama, vyakula, mziki mnene, ndani ya miezi mitatu. Hadi nikauza magari yangu Crown, Land Cruiser na nikabakia na deni kama la Sh8 milioni ambazo nilikuwa nimekopa,” anasema na kuongezea.

“Nilikuwa nina asilimia 99 kupita kwenye uchaguzi wa mwaka huo, wakati naangalia ninavyoongoza katika kata 17 nilikuwa naongoza, nikajipa matumaini, nikaiacha familia yangu iendelee kuangalia matokeo mimi nikawa nafanya shughuli nyingine.

“Akili yangu ikawa inawaza namna ambavyo nitakuwa napiga suti za maana nikiwa naenda bungeni, lakini kuwatumikia wananchi, kwani wilaya hiyo ipo nyuma kimaendeleo.
Anasema bahati haikuwa kwake kwani ilipofika wakati wa kutangaza matokeo, akatangazwa kushinda mpinzani wake.

“Basi nikabakia nimepoa na maumivu ya kupoteza pesa, kuuza magari yangu, kilichonivuta kwenye siasa natamani Kisarawe ipate maendeleo,” amesema.

Harakati za kufanya muziki zikoje

Kingwendu anasema licha ya kutoa wimbo wa Mapepe haina maana anataka kujikita kwenye muziki, isipokuwa anafanya ubunifu wa kuchekesha watu kwa njia ya kuimba.

“Nakumbuka baada ya kutoka kwa video ya wimbo wa Mapepe, kuna mashabiki walikuwa wananishambulia mitandaoni na kuniambia wee mzee achana na kuimba hujui, jamani mimi siyo Alikiba, Diamond wala Konde Boy.

“Wapo baadhi niliwajibu, nadonyoa donyoa, hivyo watarajie kusikia nyimbo zangu za komedi, ambazo nachanganya na kizaramu, Kisukuma japokuwa mimi siyo Msukuma yaani siyo kwa maana ya kujikita kwenye mziki kabisa ni kama vichekesho,” amesema.

Siku za nyuma Kingwendu aliwahi kusema kupitia mitandao ya kijamii kuwa ana mpango wa kufanya kazi na Diamond Platnumz, kutokana na hilo Mwananchi ikataka kutambua kolabo hiyo imefikia kwenye hatua gani.

“Hiyo lazima nitaifanya, kwa sababu aliniambia anatengeneza nyimbo kali, itakayoninufaisha kwenye kazi zangu. Hivyo nangoja vitu vikae sawa na siyo huyo pekee, nitaomba kufanya na Alikiba, Konde Boy, nitajikita kwenye vichekesho zaidi, sina sauti kama zao ambazo wanaimba mapenzi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *