Samia ahimiza kuomba amani, ustahimilivuSamia ahimiza kuomba amani, ustahimilivu

RAIS Samia Suluhu Hassan amewahimiza Watanzania kuendelea kuliombea Taifa ili amani, upendo, ustahimilivu na mshikamano viendelee kudumu nchini.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema hayo alipowasilisha salamu za Rais Samia kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kisasa mkoani Dodoma jana. “Rais Samia Suluhu Hassan anawasalimu sana. Yuko pamoja nanyi, na rai yake kwa Watanzania wote ni kuendeleza maombi kwa Taifa letu kuwa watulivu na kuiombea amani iendelee kudumu,” alisema Dk Mwigulu.

Amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kulindwa na kuenziwa kwa sababu bila amani Taifa halitoweza kutekeleza majukumu yake ikiwemo fursa ya kufanya ibada na shughuli nyingine za kijamii.

“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu mengine yoyote, pasipo amani hatuwezi kuendesha ibada. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuiombea nchi yetu. Pakiwa na amani tunaweza kutekeleza yale yaliyo katika matarajio yetu, tunaweza hata kutatua yale tunayoyaona kuwa ni magumu,” alisema Dk Mwigulu.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dk Christian Ndossa. Dk Ndossa alihimiza Watanzania waishi kwa kumtanguliza Mungu, wawe na matumaini kwake na wajiepushe na maovu. Katika ibada hiyo Dk Mwigulu alifuatana na mwenza wake, Neema Nchemba. SOMA: Othman asisitiza wananchi kudumisha amani

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Pindi Chana, Mbunge wa Itigi, Yohana Msita na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *