
Idadi ya vifo kutokana na shamblio la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Ain al-Hilweh huko Sidon, kusini mwa Lebanon, imeongezeka nakufikia 13, Wizara ya Afya ya Lebanon imeripoti siku ya Jumanne jioni, Novemba 18. Jeshi la Israel, kwa upande wake, linadai kushambulia kambi ya mafunzo ya kundi la Palestina Hamas.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Israel iliendelea na mashambulizi yake ya anga nchini Lebanon siku ya Jumanne, Novemba 18, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa mwezi Novemba 2024 yaliyokusudiwa kukomesha mzozo na kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah, mshirika wa kundi la Hamas kutoka Palestine. Nchini Lebanon, jeshi la Israel kwa ujumla linadai kulenga wanachama wa Hezbollah au vituo vinavyomilikiwa na kundi hili linaloungwa mkono na Iran, ingawa pia imewashambulia wanachama wanaoshukiwa kuwa wa Hamas.
Wizara ya Ulinzi ya Lebanon imeripoti shambulio la “adui, Israel kwenye kambi ya Ain al-Hilweh huko Sidon,” ikitaja idadi mpya ya vifo ya watu13 waliouawa na wengine kadhaa waliojeruhiwa. Magari ya wagonjwa yalisafirisha majeruhi zaidi hadi hospitali zilizo karibu, kulingana na chanzo hicho.
Israel inasema ililenga “eneo la mafunzo la Hamas” Msemaji wa jeshi la Israel amesema kwamba “eneo la mafunzo la Hamas” lililengwa katika mashambulizi hayo. Hamas, kwa upande wake, imedai kwamba eneo lililolengwa “ni uwanja wazi wa michezo unaotembelewa na vijana kutoka kambini.” Mashambulizi hayo yalifanywa na ndege zisizo na rubani zilizorusha makombora matatu katika eneo lenye msikiti, bohari, na maegesho, katikati ya kambi ya Ain al-Hilweh, ambayo inapakana na jiji la Sidon, anaripoti mwandishi wetu huko Beirut, Paul Khalifeh.
Makombora hayo yalilenga gari lililokuwa limeegeshwa kwenye bohari mpoja huku watu kadhaa wakitoka msikitini, jambo linaloelezea idadi kubwa ya vifo. Miongoni mwa waliofariki ni wanachama wa Hamas pamoja na raia waliotembelea msikiti huo mara kwa mara.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Hamas imepata umaarufu katika kambi za wakimbizi za Lebanon, kinyume na chama cha Rais Mahmoud Abbas cha Fatah, ikiwa ni pamoja na eneo la Ain al-Hilweh, ambalo lina zaidi ya wakazi 70,000. Hamas inadai haina wanajeshi nchini nchini Lebanon na imekataa kushiriki katika mchakato wa kupokonya silaha kambi hizo, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Mamlaka ya Palestina na serikali ya Lebanon. Mnamo Septemba 13, malori matano ya silaha kutoka Ain al-Hilweh yalikabidhiwa jeshi la Lebanon.
Hamas yashtumu
Mamlaka na jeshi nchini Lebanon bado hawajatoa taarifa rasmi. Vyama vya kisiasa vya Lebanon na Palestina vilivyo karibu na Hamas, hata hivyo, vimelaani vikali shambulio hilo. Hamas imesema kwamba “haina vituo vya kijeshi katika kambi za Palestina nchini Lebanon,” ikiita mashambulizi ya Israel “shambulio la kinyama.” “Madai […] ya jeshi [la Israel] kwamba eneo lililolengwa lilikuwa ‘eneo la mafunzo linalomilikiwa na Hamas’ si chochote ila ni uzushi na uongo mtupu, [na] yanalenga kuhalalisha uchokozi wake wa kikatili na kuchochea chuki dhidi ya kambi na raia wetu wa Palestina,” Hamas imeandika katika taarifa.
Mapema siku ya Jumanne, Wizara ya Afya ya Lebanon iliripoti vifo viwili katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyosababishwa na Israel katika jiji la Bint Jbeil, pia kusini mwa Lebanon. Jeshi la Israel halikutoa maoni mara moja kuhusu taarifa hii.
Lebanon inawahifadhi wakimbizi wapatao 222,000 wa Kipalestina, kulingana na Umoja wa Mataifa, ambapo wengi wao wanaishi katika kambi. Chini ya makubaliano ya kimyakimya, makundi yenye silaha ya Kipalestina yanadhibiti kambi hizi, ambapo jeshi la Lebanon haliingii.