Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, amesisitiza umuhimu wa kuondolewa haraka iwezekanavyo vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa dhidi ya Iran, huku akikaribisha uwezekano wa kuondolewa vikwazo na masharti yaliyowekwa dhidi ya Tehran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, ametoa maoni kuhusu uwezekano wa Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Iran katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana (Jumatano). Amesema kuwa Beijing imekuwa ikisisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuondolewa haraka iwezekanavyo vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa dhidi ya Tehran.

Aidha, Guo Jiakun alieleza matumaini yake kwamba Iran na Marekani zitatekeleza ipasavyo makubaliano ambayo tayari wameyatia saini, zitaendelea na mazungumzo yao, na kuongeza juhudi za kufikia suluhisho la kisiasa la kina kuhusu suala la Iran kwa haraka iwezekanavyo.

Marekani na utawala wa Israel zilianzisha shambulio lao la pili dhidi ya Iran alfajiri ya tarehe 28 Februari 2026, wakati mazungumzo kati ya pande hizo yakiendelea. Baadaye, tarehe 9 Aprili 2026, ilitangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kwa upatanishi wa Pakistan, na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yakaanza mjini Islamabad.

Hatimaye, baada ya upatanishi wa Pakistan, Qatar na baadhi ya nchi nyingine za eneo, Iran na Marekani zilifikia makubaliano. Hati ya makubaliano hayo (Memorandum of Understanding) ilisainiwa kwa njia ya kielektroniki na marais wa nchi hizo mbili, Masoud Pezeshkian wa Iran na Donald Trump wa Marekani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *