Kampuni kubwa ya dawa na kemikali ya Ujerumani, Bayer, imeshutumiwa kwa kusambaza fosforasi nyeupe na glyphosate inayotumiwa na jeshi la Israel katika mashambulizi yake nchini Lebanon, na kuibua maswali mapya kuhusu mnyororo wa usambazaji wa silaha zilizopigwa marufuku zinazotumika katika uchokozi huo kuua raia wa Lebanon.

Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Germany’s Coordination gegen Bayer-Gefahren (CBG) na Medico International umefichua kwamba Bayer, ambayo ilinunua Monsanto mnamo 2018, inahusishwa na mnyororo wa usambazaji wa glyphosate na fosforasi nyeupe inayotumiwa na jeshi la Israel nchini Lebanon.

“Kuna ushahidi madhubuti kwamba fosforasi iliyotumika katika vita vya Mashariki ya Kati inatoka katika kiwanda cha uzalishaji wa glyphosate cha Bayer huko Soda Springs nchini Marekani,” mwakilishi wa CBG Jan Pehrke amesema.

Ingawa katika mkutano wa Aprili 2026 bodi ya Bayer ilikana kutuma glyphosate moja kwa moja kwa jeshi la Israel au Marekani, lakini haikukana kutoa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa fosforasi nyeupe.

Ripoti hiyo – yenye kichwa cha habari “Cartographies of Destruction: Israel’s War Against Lebanon” – inasema vikosi vya jeshi la Israel vilipanua sera ya kijeshi ambayo “ilijaribiwa” kwa mara ya kwanza katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa mnamo 2014 kwa kutumia glyphosate kama silaha nchini Lebanon.

Wizara ya Kilimo ya Lebanon iligundua viwango vya glyphosate mara 20 hadi 30 juu ya viwango vya kawaida katika sampuli za udongo zilizoathiriwa, huku Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo akielezea uchafuzi huo kama uhalifu wa “mazingira na afya”.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesajili matumizi makubwa ya fosforasi nyeupe ya Israel, ikiwa ni pamoja na huko Gaza baada ya Israel kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika eneo hilo baada ya Oktoba 7, 2023. Human Rights Watch imethibitisha kuwa Israel imetumia fosforasi nyeupe katika kwa uchache manispaa 17 za Lebanon tangu Oktoba 2023.

Mnamo Aprili 2026, Wizara ya Mazingira ya Lebanon iliikosoa Israel kwa kufanya “kitendo cha mauaji ya kimbari,” ikikadiria hasara ya mazingira iliyosababishwa na fosforasi nyeupe za Israel kuwa dola bilioni 25 baada ya maelfu ya hekta za misitu kuharibiwa na kusababisha uchafuzi mkubwa wa udongo na “kubadilisha mandhari ya kidhahiri na kiikolojia” ya kusini mwa Lebanon.

Matokeo hayo yameimarishwa na uchunguzi wa New York Times uliochapishwa mnamo Juni 6, ambao ulithibitisha kwamba Israel ilitumia mara kwa mara fosforasi nyeupe katika maeneo yenye watu wengi ikiwa ni pamoja na Tyre, Nabatieh, Qlayaa, Khiam na Yohmor.

Itakumbukwa kuwa Ujerumani ilikuwa miongoni mwa nchi za Magharibi zilisaidia mpango wa silaha za kemikali wa Iraq wakati wa vita vya Iraq vya 1980-88 dhidi ya Iran, huku makampuni ya Ujerumani yakichukua nafasi muhimu katika kuipatia serikali ya Saddam Hussein teknolojia, vifaa na zana zilizohitajika kutengeneza silaha za kemikali.

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *