
Afrika Kusini inajiadaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa G20, unaowakutanisha viongozi kutoka mataifa tajiri duniani, kujadili masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumu na kisiasa, hata hivyo Marekani haitawakilishwa katika mkutano huo wa Jumamosi na Jumapili.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kuelekea kufanyika kwa mkutano huu, ambao Afrika Kusini ni mwenyeji kwa mara ya kwanza, rais Donald Trump alitofautiana na mwenzake Cyril Ramaphosa kuhusu ajenda ya kikao hicho.
Afrika Kusini inalenga kutumia mkutano huu kushinikiza mataifa tajiri, kuhakikisha kuwa mataifa yenye uchumi mkubwa yanatoa mikopo yenye masharti kwa mataifa yanayoendelea, lakini pia kuhakikisha kuwa, kuna usawa kwenye masuala mbalimbali ikiwemo vita vya mabadiliko ya tabia nchi.
Suala lingine ambalo limeifanya Marekani kususia mkutano huu, ni madai kuwa Afrika Kusini inakiuka haki za Wazungu walio wachache nchini humo, maarufu kama Afrikaners, kwa madai kuwa wanauawa na kunyanyaswa.
Aidha, mkutano huu unakuja wakati huu Marekani ikiiwekea Afrika Kusini, nyongeza ya asilimia 30 ya ushuru kwa bidhaa zake zinazoingia nchini humo.
Rais Ramaphosa hata hivyo amesema hatua ya Marekani kususia mkutano huo, itakuwa ni hasara kwao.
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa, kutokuwepo kwa Marekani, kutatoa fursa kwa China, ambayo itawakilishwa na Waziri Mkuu Li Qiang, kutawala mazungumzo hayo na kushawishi uungwaji mkono wa sera zake.