Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha mshereheshaji na mchekeshaji maarufu nchini Emanuel Mathias (Mc Pilipili), Mshereheshaji Anthony Luvanda (Mc Luvanda) ameibua mjadala mpya kuhusu usalama wa watu maarufu.

Akizungumza jijini Dodoma alipofika kutoa pole msibani, Luvanda amesema mazingira ya sasa yamebadilika. Na yanaonyesha wazi umuhimu wa wasanii na watu wengine maarufu kuwa na ulinzi wa kitaalamu au vifaa vya kiusalama vinavyoweza kusaidia katika dharura.

Akiwa amejawa na simanzi, MC Luvanda amekiri kuwa awali alikuwa akiwakosoa viongozi wa dini na watu mashuhuri waliokuwa wakitembea na walinzi binafsi. Lakini sasa anaona mantiki ya hatua hiyo. 

“Kwa hali ilivyo sasa, lazima tuwe na walinzi si lazima bodyguard wa nguvu. Bali mtu mwenye ujuzi wa usalama. Kwa wenzetu kuna kifaa kinachoitwa panic button, ukibonyeza tu, mtu aliye mbali anapata taarifa kuwa uko hatarini,” amesema

Luvanda amesema kuwa teknolojia inaweza kuwa mkombozi kwa watu maarufu, akitaja uwepo wa tracking devices na hata microchip zinazoweza kusaidia kujua mahali mtu alipo pindi anapokumbana na hatari.

Utakumbuka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gallus Hyela alisema wameshirikiana na madaktari katika kuufanyia uchunguzi mwili wa MC Pilipili na kubaini kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida hivyo wameanza uchunguzi mara moja kubaini waliohusika.

“Ni kweli, tumeshirikiana na wataalamu ambao ni madaktari, mwili ule tumebaini ulikuwa na alama zinazoonyesha kulikuwa na shida ambayo ni kipigo. Maana alama zile hawikuwa za kawaida, hivyo tumeanzisha uchunguzi mara moja kujua nini kilitokea na tungeomba yeyote mwenye taarifa za siri juu ya jambo hilo atupatie,” amesema Hyela.

Mwili wa MC Pilipili ulipokelewa siku ya Jumapili Novemba 16,2025 majira ya saa 11 jioni katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo inaelezwa kuwa ulipelekwa na wasamalia wema. Unatarajia kuzikwa leo Novemba 20,2025

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *