
Zurich, Switzerland. Wakati nchi sita zitakazocheza hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026, wawakilishi wa Afrika, DR Congo wametengenezewa mazingira rafiki katika kinyang’anyiro hicho.
DR Congo imepata urahisi katika mechi za mchujo wa mabara zitakazochezwa Machi mwakani huko Mexico, baada ya kupangwa katika chungu cha kwanza, jambo ambalo limeifanya itinge moja kwa moja hatua ya fainali.
Kuwekwa kwa DR Congo katika chungu cha kwanza ambacho kitakuwa pia na Iraq, kumetokana na timu hizo kuwa katika nafasi za juu zaidi kwenye chati ya ubora ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kulinganisha na nyingine nne ambazo zimewekwa katika chungu cha pili.
Ugumu zaidi upo katika timu za chungu cha pili ambazo ni Bolivia, Jamaica, Suriname na New Caledonia ambazo zitalazimika kucheza kwanza nusu fainali kusaka timu za kuingia fainali ambayo zitawania nafasi mbili dhidi ya DR Congo na Iran.
Iran itacheza na mshindi wa nusu fainali moja kusaka tiketi moja ya Kombe la Dunia kama ambavyo itakuwa kwa DR Congo.
Suriname imemaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi A la kanda ya CONCACAF lililoongzwa na Panama iliyofuzu wakati huo Jamaica yenyewe imeingia mchujo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi C la kanda yake nyuma ya vinara Curacao.
Kutoka Kanda ya CONMEBOL ambayo inawakilisha nchi za Bara la Amerika Kusini, timu iliyoingia hatua ya mwisho ya mchujo ni Bolivia.
Mshindani mwingine ambaye anaweza kukutana na DR Congo katika fainali ni New Caledonia, timu inayotokea katika Kanda ya Soka ya Oceania.
DR Congo inasaka kwa mara ya pili tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo mwaka 1974 ilipoishia hatua ya makundi.