
Ripoti hii imeandaliwa kwa kuchanganua data za kimataifa kuhusu mateso ya wanawake, ikifichua hali halisi ya tatizo ambalo limeendelea kudhoofisha usalama, afya na utu wa wanawake duniani.
Takribani mwanamke 1 kati ya 3 duniani ,zaidi ya milioni 840 amewahi kukumbana na ukatili wa kimapenzi au kijinsia kutoka kwa mwenzi, kiwango ambacho hakijabadilika tangu 2000. Katika mwaka uliopita, milioni 316 (11%) walipitia ukatili wa wenzi wa karibu, huku kupungua kwa tatizo hilo kikiwa kidogo sana kwa miaka 20. Ripoti pia inaonesha kuwa wanawake milioni 263 wamekumbana na ukatili wa kingono kutoka kwa wasiokuwa wenzi tangu wakiwa na umri wa miaka 15, ingawa idadi halisi huenda ni kubwa zaidi kutokana na unyanyapaa na hofu ya kuripoti.
“Ukatili dhidi ya wanawake ni mojawapo ya dhuluma za zamani na zilizoenea zaidi katika historia ya binadamu, na bado ni kati ya zinazopatiwa hatua chache, hakuna jamii inayoweza kujiona kuwa yenye haki, salama au yenye afya wakati nusu ya watu wake wanaishi kwa hofu. Kukomesha ukatili huu si suala la sera tu; ni suala la utu, usawa na haki za binadamu. Kila takwimu inawakilisha mwanamke au msichana ambaye maisha yake yamebadilishwa milele. Kuwawezesha wanawake na wasichana si chaguo, ni sharti kwa amani, maendeleo na afya. Dunia salama kwa wanawake ni dunia bora kwa wote.” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.
Jitihada zinazokabiliwa na ukata wa ufadhili wakati mahitaji yakiongezeka
Ripoti hii, iliyotolewa kabla ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake tarehe 25 Novemba, ni utafiti mkubwa zaidi kuwahi kufanywa kuhusu aina kuu mbili za ukatili dhidi ya wanawake. Imechambua data za 2000–2023 kutoka nchi 168 na kubainisha kuwa tatizo hili limepuuzwa sana na halipati ufadhili wa kutosha. Ingawa kuna mikakati inayothibitishwa kusaidia kuzuia ukatili, ripoti inaonya kuwa ufadhili unazidi kuporomoka, huku dharura za kibinadamu, mabadiliko ya teknolojia na ukosefu wa usawa wa kijamii vikiongeza hatari. Mwaka 2022, programu za kuzuia ukatili zilipokea ni 0.2% tu ya msaada wa maendeleo duniani, na kiwango hiki kimeendelea kushuka hadi 2025.
Hatari pana na za maisha yote
Wanawake wanaopitia ukatili wako katika hatari kubwa ya kupata ujauzito usiotarajiwa, magonjwa ya zinaa na msongo wa mawazo, na huduma za afya ya uzazi ni muhimu kwa kuwasaidia. Ripoti inaonesha kuwa ukatili huanza mapema na kuendelea maisha yote; katika mwaka mmoja uliopita, wasichana balehe milioni 12.5 (16% ya wenye umri 15–19) walipata ukatili kutoka kwa wenzi wao wa karibu. Ingawa tatizo hili lipo duniani kote, linawaathiri zaidi wanawake katika nchi maskini, zenye migogoro au zilizo hatarini na mabadiliko ya tabianchi. Eneo la Oceania (bila Australia na New Zealand) lina kiwango cha 38% cha ukatili wa wenzi wa karibu—zaidi ya mara tatu ya wastani wa dunia cha 11%.**
Wito wa kuchukua hatua na uwajibikaji
Ingawa nchi nyingi sasa zinakusanya data kuboresha sera za kukomesha ukatili, bado kuna mapungufu makubwa, hasa kuhusu ukatili wa kingono kutoka kwa wasio wenzi na makundi ya pembezoni kama wanawake wa jamii za asili, wahamiaji na wanawake wenye ulemavu, pamoja na data kutoka maeneo yenye migogoro. Mafanikio yanaonekana pale ambapo kuna dhamira ya kisiasa; kwa mfano, Cambodia inaboresha sheria, huduma, makazi salama na matumizi ya teknolojia ili kuzuia ukatili. Vilevile, Ecuador, Liberia, Trinidad na Tobago na Uganda zimeunda mipango ya kitaifa yenye bajeti maalum, hatua ambazo zimeongeza ufadhili wa ndani licha ya kupungua kwa misaada ya kimataifa.
Ili kuharakisha maendeleo ya kimataifa na kubadili maisha ya wanawake na wasichana wanaoathirika, ripoti inatoa wito kwa serikali kuchukua hatua na kutoa ufadhili wa:
- kuimarisha programu za kuzuia ukatili zenye ushahidi
- kuimarisha huduma za afya, sheria na kijamii zinazoweka manusura kwanza
- kuwekeza katika mifumo ya data kufuatilia maendeleo na kufikia makundi yaliyo hatarini zaidi
- kutekeleza sheria na sera zinazowawezesha wanawake na wasichana
Ripoti hii imezinduliwa pamoja na toleo la pili la mfumo wa ‘RESPECT Women’,unaotoa mwongozo mpya wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, hata katika mazingira ya dharura. Inasisitiza kuwa huu si wakati wa ukimya viongozi wanapaswa kuchukua hatua thabiti sasa ili kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.