Mwaka 2015, Tanzania iliandika historia mpya baada ya kuzinduliwa kwa kiwanda kipya cha kuzalisha bidhaa za kibailojia (viuadudu na viuatilifu hai) vinavyotumika katika kuangamiza viluilui wa mbu na wadudu waharibifu wa mazao ikiwa ni juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya malaria na magonjwa mengine yanayosambazwa na mbu.

Kiwanda hicho ni Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo katika eneo la Viwanda la TAMCO lililopo Kibaha mkoani Pwani ambacho ni cha kwanza Tanzania na Afrika kuzalisha viuadudu na viuatilifu hai vya kibailojia ambavyo havina kemikali kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

TBPL ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambapo Serikali ya Tanzania ndiyo mmiliki. TPBL inazalisha viuadudu na viuatilifu hai vinavyojulikana kibiashara kama BACTIVEC®, GRISELESF® na THURISAVE-24 kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Bidhaa hizi zina ufanisi wa hali ya juu katika kuangamiza mazalia ya mbu pamoja na kupambana na wadudu waharibifu bila kuathiri afya ya mlaji na mazingira. Aidha, bidhaa hizi ni mahsusi kudhibiti mdudu husika pasipo kuleta madhara kwa viumbe hai wengine hivyo hutuhakikishia utunzwaji na uendelezwaji wa baioanuai.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kaimu Meneja Masoko wa TBPL, Pilly Abbas anasema wazo la kuanzishwa kwa kiwanda hicho lilitoka kwa Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.

“Wazo la kuanzishwa kwa kiwanda hiki lilitoka kwa Mhe. Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete mara baada ya kufanya ziara nchini Cuba na kushuhudia namna nchi hiyo ilivyoweza kuzuia malaria,” amesema Pilly.

Anaongeza kuwa “aliporudi nchini alitoa maagizo kwa wizara husika kukutana na wataalamu wa Cuba kwa ajili ya kupata teknolojia hiyo kisha kuanza mchakato wa kufungua kiwanda chetu wenyewe, ndipo Serikali ikaanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda ambao ulikamilika Julai 2015 na yeye mwenyewe akaja kukizindua,” anasema Pilly.

Anasema kiwanda hicho kinatumia teknolojia ya kisasa kutoka Cuba ambapo awali wataalamu kutoka katika nchi hiyo walikuja na kutoa mafunzo kwa Watanzania ambao hivi sasa asilimia kubwa ndiyo wanaendesha shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho.

“Wenzetu kutoka Cuba walitusaidia kipindi cha mwanzoni kutoa mafunzo kwa Watanzania ambao hivi sasa ndiyo wanafanya kazi za uzalishashaji wa bidhaa hapa kiwandani,” anasema Pilly.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu alipofanya ziara kwenye kiwanda cha TBPL kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Bidhaa za TBPL: Faida kwa afya na mazingira

TBPL inajulikana kwa uzalishaji wa bidhaa BACTIVE, GRISELESF® na THURISAVE-24. Bidhaa hizi zimetengenezwa mahsusi kuondoa mnyororo wa ukuaji wa mazalia na   katika hatua zao za mwanzo ambazo hazihitaji kemikali hatarishi kwa afya na mazingira.

Pilly anasema bidhaa hizi zina faida kuu mbili; kwanza, zinaangamiza wadudu waliolengwa katika uzalishaji wa dawa husika bila kuangamiza viumbe wengine na pili, zinasaidia kupunguza utegemezi wa dawa za kemikali zinazoleta madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Hii inafanya TBPL kuwa kiungo muhimu kati ya malengo ya afya ya umma (kupunguza malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu) na malengo ya kilimo endelevu,” anasema Pilly.

Bidhaa hizi ni rafiki wa mazingira na ni maalum sana kwa ajili ya kuua viluwiluwi vya Mbu, zinadhibiti kwa ufanisi aina mbalimbali za mazalia ya mbu katika maeneo ya mijini, vijijini, viwanda na utalii, hazina madhara kwa viumbe wengine na mimea, zinafanya kazi kwa ufanisi na programu za afya ya mazingira ili kudhibiti magonjwa yanayosambazwa kwa mwanadamu na mbu.

Teknolojia na uwezo wa kiwandani

Teknolojia inayotumika katika kiwanda cha TBPL inafahamika kwa jina la baiteknolojia ambayo hutumia bakteria rafiki.

Wakati wa uzalishaji, bakteria hawa hupitia katika hatua mbalimbali zinazopelekea kuongezeka kwao. Kila hatua inapimwa na kuthibitishwa ubora. Baada ya kuthibitisha ubora bidhaa huwekwa katika vifungashio tayari kumfikia mteja.

Pilly anasema uwezo wa kiwanda kwa sasa ni kuzalisha lita milioni sita za bidhaa za kibailojia kwa mwaka ambapo mpaka sasa mnunuzi mkuu wa viuadudu ni Serikali kupitia Wizara ya Afya, ambapo wanufaika na watekelezaji wa unyunyiziaji wa dawa hizi ni Halmashauri.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah (katikati, walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha TBPL wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya kiwanda hicho zilizofanyika Kibaha mkoani Pwani. Wa pili kushoto walioketi ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Nicolas Shombe.

Soko: ndani na nje ya mipaka

TBPL imepanga kuuza bidhaa zake ndani ya soko la Tanzania kama kipaumbele cha kwanza, hasa kwa programu za afya ya umma zinazohusiana na unyunyiziaji wa viuadudu (larviciding), na pia kwa wakulima wanaotafuta mbadala wa dawa za sumu.

Bidhaa za TBPL zimeanza kutumiwa katika miji na mikoa tofauti kama sehemu ya mikakati ya kudhibiti malaria na kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoambukizwa na mbu. Aidha, bidhaa hizi zimetumiwa katika nchi nyingine za Afrika, Asia na Latino Amerika.

Miaka 10 ya kuleta mabadiliko na mikakati imara

Pilly anasema katika kipindi cha miaka kumi TBPL imefanikiwa kuleta matokeo yanayoonekana: uzalishaji wa bidhaa za biolarvicides na biopesticides umesaidia kuongeza uwezo wa kitaifa wa kukabiliana na mbu, kuzalisha ajira na kuibua uwezo wa kitaifa wa utafiti na utaalamu katika sekta ya bioteknolojia.

Mfano wa hatua hizo ni makubaliano yaliyofikiwa na kampuni ya Cuba, Labiofam S.A., mwaka 2025 ya kushirikiana kupanua kiwanda na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za kibaiolojia mpango ambao unasukuma TBPL kuelekea ukuaji wa uzalishaji na utafiti wa pamoja.

Pia, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilitangaza kukipatia kiwanda fedha kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa viuatilifu vya kibaolojia na bidhaa zinazotegemea bioteknolojia. Hii inaashiria msukumo na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuiweka TBPL kama mzalishaji muhimu wa bidhaa hizo nchini.

Pilly anasema TBPL inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji, kutanua msukumo wa masoko ndani na nje na kuendelea kubuni bidhaa mpya kama Mbolea hai (biofertilizers) na virutubisho vya chakula, bidhaa ambazo tayari zimewekwa katika mikakati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Kuongezeka kwa uwekezaji wa Serikali, ushirikiano wa kimataifa na sera za ununuzi wa Serikali kutatoa fursa ya TBPL kukua na kusaidia malengo ya Taifa ya kuondoa malaria na kuongeza tija ya kilimo.  

Miaka kumi ya TBPL ni hadithi ya kuvutia na mafanikio ya kiteknolojia. Kwa kuendeleza mchakato wa kuimarisha soko, kuhakikisha ufadhili wa kimkakati na kuongeza ushirikiano na wateja wa ndani na kimataifa, TBPL ni kiungo muhimu katika mustakabali wa afya ya umma na kilimo endelevu Tanzania.

Kiwanda hicho kinaonyesha mfano wa jinsi viwanda vinavyoweza kutumia teknolojia za kisasa katika kupunguza magonjwa na kukuza uzalishaji wa chakula bila kuharibu mazingira jambo linalopaswa kuungwa mkono kwa nguvu zaidi na wadau wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *