Dar es Salaam. Miaka miwili baada ya Zuchu kutambulishwa na WCB Wasafi, alionekana kuja kuwa mwanamuziki wa kike atakayeushika vizuri ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara lakini ghafla Tyla akaibuka na kupindua meza.
Hadi mwanzoni mwa 2023, ulikuwa huoni jina la Tyla katika muziki wa Afrika kwa ukubwa huo ukilinganisha na Zuchu ambaye tayari alikuwa nyimbo kubwa Afrika na hata kuwania tuzo kubwa duniani.
Wakati huo tayari Zuchu alishafanya vizuri na kolabo zake mbili na Diamond Platnumz, Cheche (2020) na Litawachoma (2020), miradi ambayo ilianza kuvusha jina lake nje ya Tanzania.
Alishafunika na wimbo wake, Sukari (2021) ambao video yake iliongozwa Afrika kwa kutazamwa YouTube mwaka huo, ukiuzidi hata ule wa Wizkid na Tems, Essence (2021) uliokuja kuwania tuzo za Grammy.
Kubwa zaidi alishawania tuzo za MTV EMAs 2022 zilizofanyika Duesseldorf, Ujerumani, ambapo alitajwa kipengele cha Best African Act akichuana na Ayra Starr, Black Sherif, Burna Boy, Musa Keys na Tems.
Zuchu aliendelea hivyo hadi kuja kuwa msanii wa kike mwenye wafuatiliaji (subscribers) wengi YouTube akiwapita mastaa wakubwa kama Yemi Alade na Tiwa Savage, wote kutokea Nigeria.
Wakati Zuchu akifanya yote hayo, Tyla, mzaliwa wa Johannesburg, Afrika Kusini, yeye bado alikuwa akijitafuta polepole huku akifanya kampeni katika nchi mbalimbali Afrika kwa lengo la kujitambulisha na kujitangaza.
Desemba 2022, Tyla alikuwapo Tanzania akifanya ziara katika vyombo vya habari, ila kutokana hakuwa na jina kubwa, uwepo wake hapa haukuzungumziwa sana ila alipopindua meza ndio watu wakashtuka ooh kumbe ndio yule!
Miezi saba baada ya Tyla kuondoka Tanzania, akaachia wimbo wake, Water (2023) ambao ulibadili kila kitu na kumfanya si kuwa msanii mkubwa Afrika tu, bali duniani akitawala chati kubwa na kushinda tuzo kubwa pia.
Water ni wimbo ulioingia chati ya Billboard Hot 100 akiwa msanii mdogo zaidi na wa pili Afrika Kusini kuingia katika chati hizo baada ya miaka 55, huku akiwa msanii namba moja wa kike Afrika katika mtandao wa Spotify.
Video yake ndio iliyofanya vizuri zaidi YouTube Afrika 2023 ikitazamwa zaidi ya mara milioni 100 ndani ya miezi mitatu tu, huku audio ikifikisha streams (idadi ya kusikilizwa) bilioni 1 huko Spotify hapo Februari 2025.
Mafanikio ya wimbo huo yalifanya Tyla kushinda tuzo kubwa – Grammy 2024, MTV VMAs 2024, tuzo mbili za Billboard 2024, pamoja na tuzo mbili za BET 2024 akiwa msanii wa kwanza Afrika kufanya hivyo.
Kubwa zaidi ni kushinda tuzo tatu kwa mkupuo za MTV EMAs 2024 zilizofanyika Manchester, Uingereza. Hizi ndio zile alizowania Zuchu 2022 lakini akashindwa kufua dafu mbele ya Burna Boy aliyeibuka mshindi.
Kwa matokeo hayo, Tyla akafikisha tuzo tatu za MTV EMAs na kuwa kinara wa ushindi Afrika kwa tuzo hizo sawa na Diamond aliyeshinda tatu pia ila kwa misimu miwili (2015 & 2023), baada ya kuwania mara tano.
Pia Tyla aliandika rekodi kama Mwafrika wa kwanza kushinda kipengele cha Best R&B ndani ya MTV EMAs, hivyo kwa ujumla akiungana na kina Whitney Houston, Jennifer Lopez, Alicia Keys, Beyonce Knowles n.k.
Kwa sasa Tyla anayewania Grammy 2026, ndiye mwanamuziki wa kike anayeongoza kusini mwa Sahara kuwa na wafuatiliaji wengi YouTube – milioni 5.2, akimshusha Zuchu hadi nafasi pili akiwa na milioni 4.3.
Ni wazi mafanikio ya ghafla yake Tyla aliyetokea nyuma, yamemtisa Zuchu ambaye alishaanza kuwazidi kete mastaa wa Nigeria ambao ndio hasa wanatawala soko la muziki Afrika.
Hii ndio sababu mara nyingi Zuchu hata na mashabiki zake humuita ‘Malkia wa Muziki Afrika Mashariki’ na sio Afrika au kusini mwa Sahara!
Hiyo sio kwa bahati mbaya, wanajua kuna Tyla ambaye kiukweli hata huko Nigeria wanamuogopa kiasi kwamba hawaamini kama ni uwezo wake binafsi bali wanadai ni pandikizi (industry plant) la kuwashusha.
Ni Tyla ambaye baada ya kumaliza masomo ya sekondari 2019, alijikita rasmi kwenye muziki huku akiendelea na chuo. Alipoachia wimbo wake, Getting Late (2021) akimshirikisha Kooldrink, Epic Records walimsaini na ukawa mwanzo wa mafanikio yake.