London, England. Arsenal inaikaribisha Tottenham Hotspur leo katika Uwanja wa Emirates kuanzia saa 1:30 usiku ukiwa ni mchezo ambao hauishii katika mahitaji ya pointi tatu bali pia kuashiria utawala wa Kaskazini mwa London.

Ni mechi ya Watani wa Jadi wa London Kaskazini ambao wanakutana wakiwa wanapishana kwa tofauti ya pointi nane ambazo zinaweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na matokeo ya leo.

Arsenal ambayo ni mwenyeji wa mechi ya leo, ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na pointi 26, ikiipiku Spurs ambayo ina pointi 18.

Itakuwa ni mechi ya kwanza ya Watani wa Jadi wa London Kaskazini katika EPL kwa Meneja wa Spurs, Thomas Frank ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia Brentford.

Frank mbali na kusaka ushindi wa kwanza katika mchezo baina ya timu hizo, anahitaji ushindi pia ili kuhitimisha unyonge ambao Spurs imekuwa nao dhidi ya Arsenal kwenye mechi za Ligi Kuu England za miaka ya hivi karibuni.

Mfano ni mechi tano zilizopita za EPL baina ya timu hizo ambapo Arsenal imepata ushindi mara nne na kutoka sare moja huku ikifunga mabao 10 na Spurs yenyewe imepachika mabao matano.

Kiujumla Arsenal ni mtemi wa Tottenham Hotspur kwani katika michezo 66 ambayo timu hizo zimewahi kukutana kwenye EPL, Arsenal imepata ushindi mara 27, Spurs imeshinda mechi 15 na mechi 24 zilimalizika kwa matokeo ya sare.

Refa aliyepangwa kushika filimbi katika mechi ya leo ni Michael Oliver ambaye atasaidiwa na Marefa Wasaidizi, Stuart Burt na James Mainwaring.

Wenyeji Arsenal wanaingia katika mchezo wakimkosa Gabriel Magalhaes huku Noni Madueke, Martin Odegaard, Kai Havertz, Riccardo Calafiori na Gabriel Martinelli wakiwa kwenye hatihati.

Wageni Spurs wamepata habari njema ya kuwa fiti kwa Lucas Bergvall, Archie Gray, Mohammed Kudus, Randal Kolo Muani na  Pape Matar Sarr ambao wote wanaweza kutumika katika mechi ya leo.

Kwenye Uwanja wa Elland Road huko Leeds, wenyeji Leeds United watakuwa wakijaribu kuondoka katika nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi wakati watakapoikaribisha Aston Villa.

Kabla ya mechi za jana walikuwa katika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa EPL wakiwa na pointi 11 ambazo zilikuwa ni mbili tu juu ya zile za Nottingham Forest iliyokuwa nafasi ya 19.

Aston Villa ina pointi 18 na ushindi wa leo ugenini utaiweka katika mazingira mazuri katika kinyang’anyiro cha kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *