Congo. Kwa zaidi ya miaka 48 sasa, jina la Koffi Olomide limeendelea kuvuma ndani na nje ya mipaka ya Afrika kama moja ya alama za muziki wa DR Congo.

Umahiri wake katika kutengeneza midundo ya soukous, rhumba na ndombolo pamoja na uwezo wake wa kuongoza makundi ya wanamuziki na kuandaa maonyesho makubwa umemfanya kuwa mmoja wa wasanii wenye umaarufu mkubwa Afrika na mataifa mengine ya Ulaya kama Ufaransa.

Ngoma zake na aina ya uchezaji wa taratibu vimemfanya mkali huyo ‘Papa Ngwasuma’ kupendwa na mashabiki mbalimbali Afrika na nchi nyingine kama Ufaransa.

Hata hivyo, umaarufu wake umekuwa ukizongwa na tuhuma nzito za ukatili wa kingono, ubakaji na udhalilishaji wa madansa.

Hapa tunakuletea miaka 48 ya muziki wa Koffi na tuhuma zilivyotishia kuharibu taswira ya muziki wake, ingawa ameendelea kubaki yuleyule kimuziki.

OLO 01

Koffi alianza safari ya muziki miaka ya 1970. Aliwavutia wengi kutokana na kipaji chake cha kuandika mashairi yenye hisia, uwezo wa kupanda na kushuka kwa sauti na mtindo wa kipekee wa kutengeneza muziki wa kupendeza masikioni na wenye ujumbe unaogusa jamii. Miaka ya 1980 na 1990 alifanikiwa kuanzisha lebo yake ya Quartier Latin International, bendi iliyoibua vipaji vikubwa kama Fally Ipupa, Ferre Gola na wengine wengi.

Hilo lilimpa sifa kubwa Koffi na kumuweka katika nafasi kama mmoja wa watu waliochangia kukuza vipaji na kutazamwa kuwa mwalimu, msimamizi na kiongozi wa muziki DR Congo.

Kazi zake kama Loi, Effrakata, Danger de Mort, Force de Frappe na Haut de Gamme zilimfanya kuwa mfalme wa midundo ya dansi ya Afrika ya Kati. Mamilioni ya mashabiki walijaa katika maonyesho ya moja kwa moja Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Afrika.

Uongozi wake kisanaa uliweza kufananishwa na ule wa wanamuziki kama Papa Wemba watu walioleta mapinduzi ya muziki na mavazi, na kubadilisha kabisa ramani ya muziki wa DRC.

Ndani ya miaka 48 kwenye gemu ya muziki, Koffi ametoa albamu 32 ikitajwa kama moja ya wasanii walioachia albamu nyingi Afrika.

OLO 02

Albamu ya kwanza – Ngounda aliyoiachia 1983, Elengi (1983), Moto na Kanga (1984),13e Apôtre (1985) Haut de Gamme: Koweït, Rive Gauche (1987), Noblesse Oblige (1989), L’ombre et la lumiere (1990), Magie (1992), Danger de Mort (1993), Loi (1994), V12 (1995),Affaire d’État (1996), Pona Yo (1997), Attentat (1998), Tshala Muana (1999), Boma Nga Nélée (2000), Effrakata (2001), Fleche Ingeta (2002), Au Nom de L’Amour (2003).

Koffi (2004), Danger de Mort 2 (2005), Bord Ezanga Kombo (2006), L’Album du Siècle (2007), Abracadabra (2008), Effrakata 2 (2009), La Vie Est Belle (2010), Obsession (2011) 13eme Apôtre 2 (2012), Nollywood (2013), Bord Ezanga Kombo 2 (2014), V12 Reloaded (2015) na Nyoka Longo (2016).

Mbali na albamu hizo, lakini amefanya kolabo na wasanii wakubwa akiwemo Fally Ipupa aliyemtambulisha kwenye gemu mwenyewe, Akon wa Marekani, Soprano wa Ufaransa na wengineo.

Kwa hapa Bongo, Koffi amefanya kolabo tatu na Diamond Platnumz zilizotoka na ngoma kama Waah, Achii na Nyonga pia alifanya na Nandy ngoma ya Leo Leo ambazo zote zilipata mapokezi makubwa na kufanya vizuri kwenye mitandao.

OLO 03

MUZIKI WAKE

Koffi sio tu mwimbaji ni mtunzi, mtayarishaji wa muziki na msanii wa maigizo. Ametajwa mara kadhaa kuwa mbunifu wa mtindo wa ‘Tcha Tcho’, sauti inayobeba urahisi wa kusikika, mapenzi na mandhari za maisha ya kila siku.

Aidha Koffi alikuwa sehemu muhimu ya harakati za La Sape  kama balozi wa mavazi na urembo ya nchini DRC Congo. Kila vazi alilovaa jukwaani lilikuwa na utambulisho.

Jezi kali, viatu vinavyong’ara, kofia za kipekee na miwani ya kifahari. Alionekana msanii anayejua mitindo tofauti na kutajwa kuwa mmoja wa wakongwe wa muziki wanaoendana na sanaa. Koffi anatazamwa kwa upande mwingine sio tu msanii, bali pia balozi wa utamaduni wa Afrika, fahari ya DR Congo na alama ya kizazi kinachokwenda na wakati.

OLO 04

Ubora wa kazi zake unathibitishwa na tuzo mbalimbali alizozipata ikiwemo zile za AFRIMA akinyakua tuzo ya Legend Award mwaka 2021, tuzo ya heshima ambayo inatambua mchango wake wa muda mrefu katika muziki.

Tuzo nyingine ni International Reggae & World Music Awards (IRAWMA) alishinda Best Soukous Song kupitia wimbo wa Selfie kwenye IRAWMA, Mundi Music Awards akishinda kipengele cha Best Legendary Artist of the Year mwaka 2024.

OLO 05

MRITHI WA PAPA WEMBA

Unaweza kusema Koffi ni moja ya warithi wa nguli wa zamani Papa Wemba hasa katika mtindo wa muziki wa Soukous / Rumba ya Congo, na kwa kuwa ni mmoja wa mastaa walioendeleza urithi huo wa muziki wa kizazi cha zamani.

Papa Wemba alikuwa kiongozi wa mtindo wa Rumba Congolaise  Soukous, mtindo wa kizazi cha miaka ya 70 na 80 uliochanganya taratibu za muziki wa kiasili na vaibu ya kisasa.

Koffi alijifunza mtindo huo na kuuboresha kwa vipengele vya Ndombolo, mtindo wa kucheza wa kizazi cha 90 na watoto wa 2000 unaojulikana zaidi barani Afrika.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali hadi mwaka huu mkongwe huyo wa muziki anakadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Sh44 bilioni.

Kiasi hicho kinajumuish mali anazomiliki kama magari ya kifahari, nyumba ikiwemo iliyopo Ufaransa na dili mbalimbali za matangazo anazopiga pesa.

Licha ya kuwa na pesa na utajiri huo, lakini hakuna taarifa zaidi kama msanii huyo hutoa kwa jamii zaidi ya kugawa magari ya kifahari kwa watu wake wa karibu kama madansa.

OLO 06

TUHUMA ZA UBAKAJI

Pamoja na mafanikio haya nyota yake imekuwa ikizongwa kwa muda mrefu na tuhuma nzito za kuwafanyia ukatili watu hasa wale wa karibu kama dansa.

Moja ya tuhuma iliyochafua taswira ya muziki wa Koffi ni mwaka 2000 ile iliyomhusisha na msichana mdogo wa miaka 15 kutoka kundi lake la wachezaji. Tuhuma hizo zilifuata safari za kimataifa za bendi yake, ambapo ilidaiwa msichana huyo alinyanyaswa kingono na kushurutishwa kimwili.

Mwaka 2019 mahakama ya Ufaransa ilimkuta na hatia katika ubakaji na ikahukumiwa kifungo cha nje. Ingawa hakutumikia kifungo cha gerezani hukumu hiyo ilitikisa taswira yake kimataifa.

Haikuchukua muda na mwaka 2021 ilizuka kesi nyingine ya madai ya kuwafungia madansa wake kinyume cha sheria wakati wa ziara za kimataifa na walitishiwa na kushinikizwa.

Mahakama ya Rufaa ya Ufaransa ilimtoa hatiani kwenye tuhuma za ubakaji, lakini ikamhukumu kwa kuwanyima uhuru wachezaji hao kosa ambalo lilichukua nafasi ya juu katika msuguano wake wa kisheria.

Mbali na kesi hizo kuna lile tukio video iliyosambaa  mitandaoni akimpiga teke dansa wake katika Uwanja wa JKIA Nairobi, Kenya  iliyosababisha kukamatwa kwake na kufukuzwa nchini humo.

Malalamiko ya ndani ya bendi kuhusu udhalilishaji, lugha kali na unyanyasaji ni miongoni mwa matukio yaliyoitesa taswira ya Koffi na muziki wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *