Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Faustina Mfinanga maarufu Nandy anazidi kuthibitisha kuwa ushirikiano baina ya wasanii wa kike katika muziki ni jambo linalowezekana na lina faida kubwa tofauti na mtazamo uliodumu kwa miaka mingi ndani ya tasnia.

Kwa muda mrefu ilizoeleka kuona ushirikiano zaidi ni kati ya wasanii wa kiume au kolabo za msanii wa kike na wa kiume, huku ule wa wanawake kwa wanawake ukionekana kuwa finyu.

Utakumbuka Nandy alijitambulisha rasmi kwenye muziki kupitia wimbo wake Nagusagusa (2016), hatua iliyomfungulia milango ya mafanikio makubwa na sasa akitambulika kama chapa yenye ushawishi.

Tangu wakati huo ameendelea kufanya vizuri akitoa albamu moja, The African Princess (2018) pamoja na EP tatu zilizofanya vizuri; Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022).

Ndani ya miaka miwili iliyopita Nandy ameshirikishwa zaidi na wasanii wenzake wa kike baadhi yao wakiwa ni Lulu Diva (Mtaalamu 2023), Mimi Mars (Pole 2024), Yammi (Lonely 2024) na Maua Sama katika kibao cha Poa kilichotoka 2024.

Wakati kwa muda mrefu ikionekana kuwa nadra sana kushuhudia msanii wa kike akitoa au akishiriki katika miradi mingi mfululizo pamoja na wanawake wenzake, kwa Nandy imekuwa tofauti kidogo.

Katika mazingira ya Bongofleva, wasanii wa kike mara nyingi huonekana kuwa kwenye mashindano yasiyo ya lazima, jambo linalobana fursa ya kufanya kazi kwa pamoja.

Wengi hutajwa kuwa na malengo binafsi yanayopingana, mazingira ya ushindani, au hata kuwa hofu kwamba kushirikiana kunaweza kupunguza muonekano au nguvu ya chapa ya msanii husika. Mathalani, mwimbaji Dayna Nyange amewahi kutaja wazi kuwa hajawahi na hana mpango wa kumshirikisha msanii wa kike katika nyimbo zake kwa sababu anahisi muziki wake hauhitaji hilo.

Kauli ya Dayna aliyetoka na ngoma zake kama Mafungu (2009) na Nivute Kwao (2011), inaonyesha wazi ni kwa namna gani kila msanii anavyojenga falsafa yake binafsi kuhusu ushirikiano. Hata hivyo, sio wasanii wote wanaona hivyo. Rapa Rosa Ree, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliowahi kushirikiana na wanawake wengi katika kazi zake na za kwao pia, yeye ana mtazomo tofauti.

Rosa Ree ambaye ameshirikiana na Nandy katika wimbo Dah Remix (2024), anasema hajawahi kuona ugumu wa kufanya kazi na wenzake. “Binafsi nashirikiana na wasanii wenzangu wa kike na nafurahi sana pale ambapo nafanya kazi na mwanamke mwenzangu ambaye ana malengo, ana ndoto na ana uwezo mkubwa katika sanaa.

“Na hii nimeiona kwa wasanii wengi wanaochana kama mimi, na hata waimbaji kama Ruby na Maua Sama ambao nilifanya nao kazi kipindi cha nyuma. Kwangu mimi napenda kushirikiana na wenzangu,” anaeleza Rosa Ree.

Mkali huyo wa kibao, Dip n’ Whine It (2019), ni miongoni mwa wasanii waliothibitisha kuwa hamasa ya wanawake kufanya kazi pamoja ipo, endapo tu watapata mazingira na nia ya kujenga kitu kizuri.

Moja ya nyimbo zake zilizohusisha wasanii wa kike ni ‘Threesome’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Goddess (2022), ambapo aliwashirikisha Frida Amani na Chemical. Wimbo huo ulipokewa vizuri na mashabiki na hata kutajwa kuwa moja ya miradi iliyodhihirisha kuwa wanawake wakiungana wanaweza kutoa kazi zenye ubora wa kiwango cha juu.

Kwa upande mwingine, kiwanda cha Bongofleva kimewahi kushuhudia mafanikio makubwa kupitia kolabo za wanawake, ingawa ni chache. Baadhi ya kolabo hizo ni ‘Bounce’ ya Vanessa Mdee na Maua Sama, ‘Same Boy’ ya Linah na Recho, ‘Tabibu’ ya Grace Matata na Mwasiti, pamoja na ‘Hello’ ya Maua Sama na Grace Matata.

Hiyo ni miongoni mwa miradi iliyopokewa vizuri ikionyesha kuwa wanawake wakifanya kazi pamoja matokeo yake ni mazuri na ya kuvutia. Ingawa kwa muda mrefu kumekuwa na dhana potofu kwamba wanawake katika muziki hawawezi kushirikiana au hawataki kufanya kazi pamoja. Hata hivyo, hatua za Nandy na Rosa Ree zinaonyesha kuwa fikra hizo zinaenda zikipitwa na wakati.

Kizazi kipya cha wasanii wa kike kinaonekana kuwa tayari kuvuka mipaka ya mawazo ya zamani na kujenga ushirikiano wenye kuleta matokeo chanya katika tasnia nzima kwa ujumla.

Nandy anaendelea kutoa somo muhimu – kuwa mwanamke katika muziki si sababu ya kuwa mpweke, bali ni nafasi ya kushirikiana, kujenga tasnia, na kuonesha kuwa wanawake wanaweza kupanga, kutekeleza na kufanikiwa miradi mikubwa pamoja. Kwa mwendo huu, huenda kesho na keshokutwa ikashuhudia wimbi kubwa la wasanii wa kike wakifanya kazi nyingi zaidi za ushirikiano. Wakivunja vikwazo na kuandika historia mpya katika muziki wa Bongo na Afrika kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *